Gavana alaumiwa kwa kuzima mashindano ya urembo kaunti

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na ALEX NJERU

GAVANA Muthomi Njuki wa Kaunti ya Tharaka-nithi amelaumiwa vikali na madiwani kwa kukataa shinikizo za kuandaa mashindano ya urembo akishikilia kuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Kwa sasa, madiwani hao wanamtaka kiongozi huyo kuelezea sababu yake kufutilia mbali mashindano hayo ambayo yalianzishwa na mtangulizi wake, Bw Samuel Ragwa.

Kufuatia hayo, madiwani wameipa kamati husika siku 14 kuwasilisha suala hilo katika Bunge la kaunti.

Madiwani hao pia wamemlaumu gavana huyo kwa kuwatowashirikisha vijana katika uongozi wake, huku wakiapa kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa mashindano hayo yamerejeshwa. Walieleza kuwa hafla hizo hukuza talanta.

Lakini akijitetea dhidi ya madai hayo, Bw Njuki alisema kuwa hataogopa vitisho vyao, kwani lengo lao ni kujipatia mamilioni ya pesa kama marupurupu. Alisema kuwa badala yake, atatumia pesa hizo kwa masuala muhimu kama afya, maji na kuimarisha hali za barabara.

“Kuna mambo muhimu sana ya kufanya, badala ya kuandaa mashindano ambayo hayatawasaidia wananchi hata kidogo,” akasema Bw Njuki.

Aliwalaumu kwa kutumia visingizio vya kuinua hadhi za vijana kujitajirisha.

Picha/ Alex Njeru

GAVANA wa Tharaka-nithi, Muthomi Njuki aungana na wachezaji ngoma wa kitamaduni wakati wa mkutano uliofanyika wadi ya Nkondi awali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.