Ajali yakatiza maisha ya 12 waliotarajia kufika Nairobi

Abiria hao walifariki basi walilokuwa wakisafiria lilipogonga lori likijaribu kulipita

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na MACHARIA MWANGI

WATU 12 walifariki basi walilokuwa wakisafiria lilipogongana na lori eneo la Sogea kwenye barabara ya Naivasha kuelekea Gilgil jana asubuhi.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo (OCPD) , Bw Emmanuel Opuru alisema basi hilo lilikuwa likijaribu kupita lori ajali ilipotokea.

Kulingana na polisi, basi lilikuwa likitoka Vihiga kuelekea Nairobi na lori lilikuwa likielekea Nakuru.

“Watu 11 walikufa papo hapo miongoni mwao wakiwa wanawake saba na wanaume wanne. Wengine wanne walipelekwa hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha,” alisema Bw Opuru.

Mwanamke mwingine aliaga dunia akitibiwa hospitalini.

Bw Opuru alisema abiria 11 walipelekwa hospitali ya Kaunti ya Nakuru na wawili walitibiwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Gilgil.

Kulingana na Bw Isaac Mbugua, aliyeshuhudia ajali hiyo basi lilikuwa likijaribu kupita gari lingine lilipogongana na lori.

Watano miongoni mwa waliokufa ni washirika wa kanisa la African Divine Church waliokuwa wametoka kwa mazishi.

Dereva wa basi hilo pia alikufa kwenye ajali hiyo.

Bi Lucy Wangui Njoroge alieleza kuwa baba yake amekuwa akiendesha basi kwa miaka mingi.

“Baba yangu amekuwa dereva wa basi kwa miaka mingi na niliwasiliana naye Jumamosi jioni akaniambia alikuwa akiondoka mjini Kapsabet,” alisema.

Kondakta wa basi hilo, Bw Isaac Mbugua, alinusurika akiwa na majeraha madogo. Alitibiwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Gilgil to kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Bw Mbugua alisema dereva alikuwa akijaribu kupita lori basi lilipogongana na lori. “Ninamlaumu dereva wa lori. Dereva wetu alipojaribu kupita lori, aliongeza kasi na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi,” alisema Bw Mbugua.

Lakini manusura mwingine, Amin Hamza aliyekuwa akielekea Nairobi kutoka Magharibi mwa Kenya alimlaumu dereva wa basi akisema alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi ajali ilipotokea.

“Dereva wa basi alikuwa akiendesha vibaya sana na dereva wa lori alijaribu kuhepa lakini hakuweza,” alisema Bw Hamza.

Alisema miongoni mwa waliokufa ni abiria wawili waliopanda gari mjini Nakuru.

Manusura mwingine, Absalom Gulundu, 72 pia alidai dereva wa basi alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi.

Mkuu wa hospitali ya Kaunti Ndogo ya Gilgil, Denver Kamau, alisema watu 29 walipelekwa hapo Jumapili alfajiri. “

Picha Ayub Muiyuro

Mabaki ya basi lililohusika katika ajali eneo la Gilgil, barabara ya Nairobi- Nakuru jana. Watu 12 walifariki.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.