Serikali yapuzilia mbali madai ya wanasiasa kuhusu usalama

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti -

Na ABDIMALIK HAJIR

KAMISHNA wa eneo la Kaskazini Mashariki, Bw Mohamed Birik, amewaambia viongozi wa kisiasa waache kulaumu serikali kuhusu hali mbaya ya usalama na badala yake wasaidie juhudi za serikali kupambana na ugaidi.

Bw Birik alishauri viongozi wa eneo hilo walio na malalamishi kuhusu jinsi shughuli za kiusalama zinavyosimamiwa watumie njia rasmi kuyawasilisha badala ya kuyapeleka hadharani.

Alisema hayo jana, siku chache baada ya viongozi kadhaa wakiwemo Gavana wa Mandera Ali Roba, Seneta wa Garissa Yussuf Haji na Mbunge wa Ijara Sofia Abdinoor, kukashifu maafisa wa usalama kwa madai kwamba huhangaisha wakazi.

Bi Abdinoor alilalamikia jinsi idadi kubwa ya wakazi wamekuwa wakitoweka kwa njia zisizoeleweka huku kukiwa na madai kwamba huwa wanachukuliwa na maafisa wa usalama.

Kwa upande wake, Bw Roba alidai wanajeshi wamekuwa wakiwahangaisha wakazi kama njia ya kulipiza kisasi kwa shambulio la bomu lililotokea majuzi katika eneo la Daba City lililo Elwak, Kaunti ya Mandera.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.