Fedheha ya Fistula yafanya wanawake kukosa matibabu

Taifa Leo - - Kurunzi Ya Pwani - NA STEPHEN ODUOR

WANAWAKE wengi katika jamii za Kaunti ya Tana River wamepoteza ndoa zao baada ya waume zao kukosa kuelewa chanzo cha uvundo wa mkojo unaoibuka kutoka kwao hasa baada ya uzazi.

Kile wasichofahamu ni kuwa wake zao wanaugua Fistula, ambayo imewafanya wengi kutengwa na jamii na kuishia kuishi maisha ya upweke, na yenye fedheha chungu nzima, mbali na gharama wanazokumbana nazo kugharamia matibabu yasiyowasaidia.

Bi Faiza, 27 ameishi kujifunga pampers kwa mwaka wa tatu sasa. Ndoa yake ilisambaratika miaka mitatu iliyopita baada ya mumewe kushindwa kuvumilia harufu wala kuelewa chanzo cha harufu hiyo.

"Baada ya kuzaa mtoto wangu wa kwanza hapa nyumbani, ndio hiyo shida ilianza, sasa nikaona iko tu sawa na sikushughulika sana, nilijua tu nitapona," alisimulia.

Lakini alivyodhania sivyo kwani hali ile iliendelea miezi kadhaa, kwani pasipo kujua, alijipata keshajiendea haja ndogo ghafla alikoketi.

Alipoamua kueleza wakongwe kijijini kuhusu masaibu yake, hawakumpa suluhisho kamili ila ganga ganga ya kumpa matumaini.

Alishauriwa kutumia maji ya chumvi, dawa za kienyeji, mafuta ya aina mbalimbali kusuluhisha tatizo lake lakini juhudi zote hazikufua dafu wala kuzalisha matumaini, kwani hali ilizidi kuzorota.

Katika kaunti hiyo hiyo, Bi Asha, 22 ameishi kupambana na fistula kwa mwaka wa tano sasa. Mbali na kujipata katika hali hiyo baada ya kujifungua nyumbani, alimpoteza mwanawe.

"Nilipoteza mtoto wangu katika hiyo hali, lakini sikujua kwamba niko na fistula mpaka miezi sita baadaye, ndio nikashuku naugua, "alisimulia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.