Zogo la kidplomasia kati ya Kenya na TZ litatuliwe upesi

Taifa Leo - - Barua -

Na CHARLES WASONGA

VITA vya kiuchumi baina ya Kenya na Tanzania sasa vimegeuka donda ndugu ambalo ukosefu wa tiba yake unatishia uhusiano wa mataifa ya jumuiya nzima ya Afrika Mashariki.

Hatua ya hivi majuzi ya serikali ya Kenya kuwekea wafanyabiashara wa Tanzania vikwazo vya kuuza bidhaa zao humu nchini ni hatua ya kulipiza kisasi baada ya serikali ya Rais John Magufuli kuwekea bidhaa za Kenya visiki kuingizwa nchini humo.

Na hapo Alhamisi, kampuni ya Safaricom ililazimika kumteua Bi Sylvia Mulinge kuwa meneja wake wa miradi maalum baada ya serikali ya Tanzania kujikokota kwa miezi mitano kumpa kibali cha kazi kujaza nafasi ya Mkurugenzi Mkuu mpya wa Vodacom Tanzania aliyopewa.

Mvutano huu wa kibiashara unajiri chini ya majuma mawili baada ya mataifa haya kukubali kuzika tofauti zayo na kushirikiana kwa karibu kibishiara.

Kizingiti kingine ni kuwa mataifa haya mawili yamewekeana vikwazo kwa raia wake kusafiri hadi taifa jirani. Hii inazuia ubadilishanaji wa nguvukazi na kunoana kimawazo kuhusu biashara.

Iwapo Jumuiya ya Afrika Mashariki inalenga kukuza ushirikiano baina ya mataifa yote sita, vita hivi baridi baina ya Kenya na Tanzania vinafaa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.

Juhudi za Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Kenya kuketi kwa meza ya mazungumzo na ile ya Tanzania ili kurudisha uhusiano mwema badala ya kutazama historia ikijirudia zimeambulia pakavu.

Hatua za hapo awali za kuwakamata ng’ombe na kuwapiga mnada, Operesheni Timuatimua, kuchoma vifaranga na malalamishi ya Tanzania kuwa Kenya haifai kujenga mradi katika Mto Mara ni ishara kuwa mvutano huu huenda unahitaji suluhu ya kimataifa na wala si ya kijumuiya.

Vikwazo hivi vinazuia maendeleo ya mataifa mengine ya jumuiya hii kufikia malengo yake ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, na sasa ni wakati wa Muungano wa Afrika (AU) kuingilia kati.

Ikumbukwe kuwa uhusiano mbovu baina ya Nairobi na Dar es Salaam ulichochea kusambaratika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mnamo 1977, hasa kutokana na tofauti za kimawazo huku kila taifa likijitahidi kulinda matakwa yake ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Iwapo viongozi wote wa Afrika watalemewa kupatanisha Kenya na Tanzania, basi itabidi Umoja wa Mataifa (UN) uingilie kati kuokoa hali kwa kuwa mataifa ya kanda hii yanategemeana kiuchumi na mataifa mawili hayafai kuruhusiwa kuhujumu maendeleo ya mataifa mengine.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.