Thiago Silva tajiri wa fedha na pumzi zisizokwisha uwanjani

Taifa Leo - - Dimba - NA CHRIS ADUNGO

KAPTENI wa Paris Saint-germain (PSG), Thiago Silva ni beki matata ambaye pia huvalia utepe wa unahodha katika timu ya taifa ya Brazil.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 huogopwa pakubwa na wavamizi wa timu zinazomenyana na PSG au Brazil kutokana na nguvu zake katika kuwakabili kwenye safu za ulinzi. Upekee wake upo zaidi katika uwezo wa kuyazima kirahisi mashambulizi ya mafowadi na kuzuia mipira kutikisa nyavu za kikosi chake kiholea.

Ushawishi wa Thiago uwanjani umemzolea utajiri mkubwa katika ulingo wa soka tangu ajitose rasmi katika taaluma ya usakataji kabumbu kwa kuvalia jezi za Fluminese na AC Milan kabla ya PSG kuzitwaa huduma zake.

Kwa mujibu wa Jarida la Celebrity Worth, thamani ya mali inayomilikiwa na Thiago inakadiriwa kwa sasa kufikia kima cha Sh7.5bilioni na kiini kikubwa cha pato lake ni mshahara wa takriban Sh1.7 bilioni ambao yeye hupokezwa kwa mwaka kwa kutandaza soka uwanjani Parc des Princes, Ufaransa. Mbali na ujira huo mnono, Thiago hujirinia donge jingine kutokana na matangazo ya kibiashara kutoka kwa kampuni zinazomtumia kama balozi wa mauzo ya bidhaa zao. Malipo anayopokea kambini mwa PSG yanamweka katika kikoa kimoja na Marquinhos, Angel Di Maria na Edinson Cavani ambao wanaufuata kwa mbali mgongo wa mchezaji ghali zaidi duniani, Neymar Jr anayedumishwa kwa yapata Sh56 milioni kila wiki.

Hadi kufikia sasa, wachezaji wengine wanaolipwa mshahara wa juu zaidi katika kikosi cha PSG ila bado wanausoma mgongo wa Thiago ni Julian Draxler na Marco Verratti anayemezewa sana na Manchester United. Ingawa mkataba wa Thiago na PSG unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa 2020, huduma za sogora huyo zimeanza kuwavutia makocha wengi wa ligi kuu za soka nchini China na Amerika kwa ahadi ya mshahara mnono zaidi.

Thiago alianza taaluma yake ya soka mnamo 2004 akivalia jezi ya Juventude inayoshiriki Ligi ya Daraja la Pili nyumbani kwao Brazil.

Katika kipindi hicho, aliwajibishwa pakubwa kama winga wa kulia ila makocha waliotambua ukubwa wa uwezo wake kwenye ngome ya kikosi wakabadili mtindo wa kucheza kwake na kumfanya kuwa beki. Alijiunga na Fluminense mnamo 2006 kabla ya kutwaliwa haraka na AC Milan ya Italia.

Thiago anamiliki majumba ya kifahari jijini Rio de Janeiro, Brazil. Mojawapo ya majengo yake ni kasri la Sh615 milioni ambalo linastahiwa pakubwa na wakazi wa janibu hizo. Jengo hilo lina bwawa la kuogelea, baa, eneo la kuegesha magari, uwanja wa tenisi na mpira wa vikapu.

Ingawa Thiago anamiliki aina nyingi za magari, baadhi ya yale anayoyapenda zaidi ni Audi, SUV, Bentley Continental GT, Ferrari 458 Spider, Range Roverevoque na Mercedes CL63. Thamani ya magari haya yote inakisiwa kufikia kima cha Sh77milioni.

Thiago ana ndugu wawili, Danila Emiliano na Erivelton Emiliano. Yeye ni mume wa ndoa tangu alishane yamini na kipusa mzawa wa Brazil, Isabele ambaye amekuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi kwa takriban miaka mitano sasa. Wawili hao wamejaliwa watoto wawili: Isago na Iago.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.