Sigurdsson ajiandaa kuitwa baba, mkewe anahudhuria kliniki

Taifa Leo - - Dimba - The Sun

MIEZI mitatu baada ya kiungo mahiri wa Everton na timu ya taifa ya Iceland, Gylfi Sigurdsson kumposa Alexandra Helga Ivarsdottir, kichuna huyo aliyetawazwa mshindi wa Miss Iceland mnamo 2008 ameanza kuhudhuria kliniki.

Sigurdsson alimvisha Alexandra pete ya uchumba mwanzoni mwa Julai 2018 baada ya kuzidiwa na kijibaridi cha ukapera. Walianza kutoka kimapenzi mnamo 2010.

Wakati huo, kidosho huyo alimtaka Sigurdsson, 29, "kutuliza boli" na kusubiri hadi mwisho wa mwaka huu kabla ya kumfunga bao litakalomweka katika ulazima wa kuanza kwenda kliniki.

Hata hivyo, muda mrefu haujapita kabla ya Alexandra kujibwaga katika mtandao wake wa Instagram, na kufichua hali yake kwa kupakia picha za ujauzito na nyinginezo alizopigwa kwa pamoja na dume lake.

Katika mahojiano yake na gazeti la wiki jana, Alexandra alikiri kuwa dume lake lilikuwa na pupa ya kujikweza hadhi ya kuitwa ‘baba wa mtu’ licha ya yeye kumsihi mara kwa mara asubiri hadi watakapouhalalisha uhusiano wao kwa kulishana yamini katika sherehe za arusi ya kukata na shoka.

Akipasua mbarika kuhusu kilichomchochea pia kuubadili msimamo wake wa awali, Alexandra alisema kuwa Sigurdsson alianza kumpangia safari nyingi za ghafla, tena za usiku, katika hoteli za haiba kubwa ndani na nje ya jiji la London kwa lengo la kumshawishi akubali utamu wa uhusiano wao ukolezwe zaidi na ujio wa kimalaika.

Tangu aridhishwe na ufundi wa Sigursson katika michuano ya chumbani isiyohitaji marefa, Alexandra alijilegeza zaidi kwa mwanasoka huyo aliyempa pete ya uchumba mnamo Julai katika visiwa vya Bahamas.

Kwa kuibuka mshindi wa Miss Iceland, Alexandra alifuzu kuwania taji la Miss World lililowakutanisha vipusa 109 nchini Afrika Kusini. Aliambulia katika nafasi ya 15 katika mashindano hayo yaliyotawaliwa na mrembo Ksenia Sukhinova wa Urusi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.