Oswago anafuata nyayo za Sanchez

Taifa Leo - - Gumzo La Spoti -

BRIAN Oswago ni kiungo wa kati anayesakatia timu ya Asek FC inayoshiriki kwa sasa michuano ya ligi Ukanda wa Kati, katika uliokuwa Mkoa wa Bonde la Ufa. Anaazimia kucheza mpira hadi afikie kiwango cha wachezaji mahiri kama akina Alexis Sanchez na Paul Pogba wa Manchester United.

Motisha yake kubwa yatokana na wingi wa mabao aliyopachika wavuni tangu msimu wa 2018-19 uanze. Ananasibisha fanaka tele aliyonayo na ushirikiano mkubwa kati yake na wachezaji wenzake pamoja na kocha Alex Angana. Akihudumu katika safu ya kati akiwa kiungo mshambulizi na wakati mwingine kiungo mkabaji, wepesi na kasi isiyo kifani kila anapodhibiti mpira ndio nguzo inayomhakikishia namba kikosini.

Alianza kucheza mpira akiwa katika shule ya msingi mtaani Shaabab, Nakuru kisha baadaye akaendeleza kipaji alipojiunga na

Shule ya Upili ya St Gabriel Lanet. Hivi sasa timu yake inashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali la michuano ya FKF.

Tayari amefunga mabao 12 kutokana na mechi 16 alizosakata. Amechangia mabao mengine manane na kutoa pasi sahihi zilizozalisha baadhi ya magoli muhimu katika timu yake. Mnamo 2014, alianza kuchezea timu ya Community FC inayopiga mazoezi katika uga wa Medical Nakuru. Baadaye akaanza kuhudumia Wembley United kabla ya kujiunga na Suapanax mnamo 2016 na kutesa sana na kuibuka mfungaji bora katika jumla ya misimu miwili. Hivi sasa anaisaidia timu yake ya Asek tangu ajiunge nayo rasmi mwanzoni mwa mwaka uliopita.

“Soka ni kama bahati nasibu. Wakati mwingine mpira unaweza ukakubali au kukataa,’’ anasema.

Mwanzoni mwa msimu huu, alisaidia timu yake kuangamiza majagina Freehold 2-0. Hatimaye, alichangia mabao mawili katika mchuano dhidi ya Posta Lanet walipoambulia sare ya 3-3. Alichachawiza watani wao wa siku nyingi Whitehouse na kutinga bao la kipekee katika mechi iliyomalizika kwa 1-0. Baadaye, alitia kimiani magoli matatu katika mechi yao na Beef Research iliyotamatika kwa wao kusajili ushindi mnono wa 6-4.

Kiungo Brian Oswago wa timu ya Asek FC, Nakuru

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.