Idadi ya walioangamizwa na Tsunami Indonesia yafika 832

Taifa Leo - - Habari Za Afrika Na Dunia -

Idadi ya watu waliouawa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini Indonesia imeongezeka hadi 832 huku wakazi wa kisiwa cha Sulawesi wakiteseka kutafuta chakula na maji na uporaji kuongezeka.

Shirika la Taifa la Mikasa lilitangaza idadi hiyo ambayo ni mara tatu iliyokuwa imetangazwa awali.

Makamu Rais wa Indonesia Jusuf Kalla alisema idadi ya waliokufa inaweza kufikia maelfu kwa sababu maeneo mengi hayajaweza kufikiwa.

"Inatisha sana,” alisema Risa Kusuma, mama mwenye umri wa miaka 35 akimtuliza mtoto wake katika kituo cha uokoaji katika jiji la pwani la Palu lililoathiriwa na tsunami hiyo.

“Kila dakika, ambulansi inaleta miili. Hakuna maji safi. Maduka yote yameporwa,” alisema.

Runinga ya Metro Indonesia, Jumapili ilionyesha picha za jamii inayoishi pwani eneo la Donggala, karibu na lilikoanzia tetemeko hilo na ambapo nyumba ziliharibiwa kabisa lakini mkazi mmoja alisema watu wengi walikuwa wamehamia eneo salama baada ya tetemeko hilo.

"Lilipotingishika kwa nguvu, sote tulikimbia milimani,” mwanamume aliyejitambulisha kama Iswan aliambia runinga ya Metro.

Rais wa Indonesia Joko Widodo alitembelea eneo hilo Jumapili alasiri kujionea uharibifu mwenyewe.

Katika jiji la Palu, misaada ilimwangika Jumapili na jeshi la Indonesia lilitumwa kuungana na waokoaji kutafuta manusura miongoni mwao watu 150 waliokuwa katika hoteli moja.

"Tulifaulu kumuokoa mwanamke akiwa hai kutoka hoteli ya Roa-roa usiku uliopita," Muhammad Syaugi, mkuu wa shirika la kitaifa la uokoaji aliambia AFP.

"Hata jana tulisikia watu wakiitana wasaidiwe,” alisema.

"Tunachohitaji sasa ni mashine makubwa kuondoa vifusi. Nina wafanyakazi wangu tayari lakini ni vigumu kutegemea nguvu zao kuondoa vifusi hivi,” alisema.

Pia, kulikuwa na wasiwasi kuhusu “Tunachohitaji sasa ni mashine makubwa kuondoa vifusi. Nina wafanyakazi wangu tayari lakini ni vigumu kutegemea nguvu zao kuondoa vifusi hivi,”

Muhammad Syaugi, Mkuu wa Shirika la Uokoaji

hatima ya mamia ya watu waliokuwa wakijiandaa kwa tamasha ufuoni wakati tetemeko hilo la kipimo cha 7.5 kwa richa lilipotokea Ijumaa na kusababisha tsunami. Shirika la Mikasa lilisema linaamini raia 61 wa kigeni walikuwa Palu tetemeko hilo lilipotokea huku wengi wao wakiwa salama.

Hata hivyo, Raia watatu wa Ufaranza na mmoja wa Korea Kusini waliokuwa wakiishi katika hoteli iliyoharibiwa hawakuwa wamepatikana.

Ndege ya kijeshi aina ya C-130 iliyotumiwa kusafirisha misaada ilifaulu kutua katika uwanja mkuu wa ndege jijini Palu, ambao ulifunguliwa kwa ndege za kutoa misaada ya binadamu.

Picha/afp

Jamaa na marafiki wa wendazao wabeba miili iliyopatikana vifusini baada ya tsunami kutokea katikati ya kisiwa cha Palu, Indonesi. Idadi ya waliouawa sasa imetimia 832 huku ikikisiwa kwamba huenda maelfu ya miili ikapatikana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.