Lipo janajike linalodai ni penzi la muhibu wangu

Taifa Leo - - Fumbo & Falaki -

Vipi shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitano na nampenda sana. Hata hivyo, kuna msichana aliyenitumia SMS juzi akaniambia kuwa ni mpenzi wake. Nilimuuliza mpenzi wangu akaniambia kuwa hana mwingine ni mimi tu. Nilimtumia SMS ya msichana huyo na nikamwambia sitakubali anichezee. Alinyamaza kidogo na akasema ni sawa. Siku iliyofuata alinitumia SMS akaniambia nikome kuwasiliana naye kwa sababu ashapata mwingine. Ajabu ni kuwa amekuwa akiwaambia binamu zake kuwa ananipenda sana lakini hataki kuongea nami. Nampenda sana na sitaki kumpoteza. Nishauri. Kupitia SMS

Kwanza, ulifanya makosa kumwamini msichana aliyedai kuwa mpenzi wa mpenzi wako. Inawezekana kuwa anammezea mate mpenzi wako na anatafuta mbinu ya kuwatenganisha ili amnyakue. Inaonekana mpenzi wako alikasirika kutokana na matamshi yako yaliyoashiria kwamba si mwaminifu kwako na hasira hizo ndizo zilizomfanya akwambie kuwa ana mwingine. Bila shaka hiyo si kweli na ndiyo maana anashikilia kuwa ni wewe tu anayependa. Ni muhimu umtafute umuombe msamaha ili kutuliza hasira zake na kufufua uhusiano wenu.

Ninashuku mpenzi wangu ana mwingine

Shangazi pokea salamu zangu. Nina mpenzi ambaye tunapendana sana ila nahofia kwamba ana mpango wa kando. Lakini kila nikimuulza hukasirika sana. Nifanye nini? Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, unashuku tu wala huna hakika kwamba mpenzi wako ana mpango wa kando. Kama una hakika ya hilo, basi achana naye. Kama huna hakika, subiri hadi utakapokuwa nayo ndipo uchukue hatua inayofaa.

Masafa baina yetu yananitia wasiwasi

Shikamoo shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 19 na nina mpenzi ambaye nampenda sana. Hata hivyo anaishi mbali nami na huwa ninamshuku. Nifanyeje? Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini unamshuku mpenzi wako. Kama huna sababu nzuri, tosheka moyoni mwako kuwa ni mwaminifu kwako na hana mwingine. Ninashuku kuwa hali yako hiyo inatokana na ule wivu wa kawaida katika mapenzi na pia kwa sababu mpenzi wako anaishi mbali nawe.

Yupo mwanamume anayenitaka mimi, 16

Hujambo shangazi. Tafadhali nahitaji ushauri wako. Mimi ni msichana mwanafunzi wa shule ya upili na nina umri wa miaka 16. Kuna mwanamume ambaye amekuwa akinisumbua akitaka tuwe wapenzi lakini mimi sina haja na uhusiano sasa kwani nimeweka mbele zaidi masomo yangu. Nifanye nini? Kupitia SMS

Kulingana na umri wako, wewe ni msichana mchanga sana tena bado unasoma. Ni jambo muhimu sana kwamba unatambua kuwa masomo yanafaa kuwa kipaumbele kwako wala si uhusiano wa kimapenzi. Mpuuze kabisa mwanamume huyo na umwambie wazi kuwa hutaki mambo yake.

Baada ya miaka 2 sasa hataki penzi

Hujambo shangazi, natumai wewe ni mzima. Nina mpenzi ambaye nampenda sana na tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Sijui amefikiria nini kwani sasa ananiambia hataki tuendelee na uhusiano na nikimuuliza sababu haniambii. Nahitaji ushauri wako. Kupitia SMS

Uhusiano, uwe wa kirafiki au wa kimapenzi ni chaguo la mtu binfasi na hakuna mikataba inayotiwa saini kudumisha mahusiano kama hayo. Inaonekana mwenzako amehisi kuwa hafurahii uhusiano wenu na ameamua kujiondoa. Hiyo ni haki yake na huwezi kumlazimisha kubakia katika uhusiano huo. Heshimu uamuzi wake na uendelee na maisha yako.

Usumbufu wake ulifanya nimteme ila anataka turudiane

Kwako shangazi. Niliachana na mpenzi wangu aliponikasirisha. Sasa ananisumbua akitaka turudiane. Nishauri. Kupitia SMS

Unafaa kuzingatia mambo mawili kuamua iwapo mtarudiana au la. Kwanza ni kitendo alichokutendea hadi ukakasirika. Je, uko tayari kumsamehe. Pili ni iwapo bado unampenda. Kama unampenda na uko tayari kumsamehe, basi fanya hivyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.