Kenya kufukuzia tiketi ya Olimpiki dhidi ya Mauritius

Taifa Leo - - Spoti - NA GEOFFREY ANENE

KENYA itaanza kampeni yake ya kutafuta tiketi ya kushiriki soka ya wanaume kwenye michezo ya Olimpiki mwaka 2020 dhidi ya Mauritius mwezi Novemba mwaka huu.

Kutokana na rekodi ya Kenya kutoshindwa katika mechi saba ambapo imekutana na wanavisiwa hawa, Emerging Stars ya kocha Francis Kimanzi itakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya vyema katika mechi za raundi ya kwanza, ambazo zitafanyika kati ya Novemba 12 na Novemba 20.

Kenya, ambayo inaorodheshwa katika nafasi ya 107 duniani, itatinga raundi ya pili ikicharaza nambari 156 duniani Mauritius. Mechi za raundi ya pili zitafanyika kati ya Machi 18 na Machi 26 mwaka 2019.

Mataifa 13 yamefuzu moja kwa moja kuingia raundi ya pili kutokana na viwango vyao bora duniani. Mataifa haya ni pamoja na Zambia, Nigeria, Algeria, Ivory Coast, Senegal, Tunisia na Morocco.

Timu saba zitakazotamba katika raundi ya tatu hapo Juni mwaka 2019, zitaungana na wenyeji wa Kombe la Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23, Misri. Mataifa yatakayomaliza Kombe la Afrika katika nafasi tatu za kwanza yatashiriki soka katika Olimpiki mnamo Julai 22 hadi Agosti 8 mwaka 2020 nchini Japan.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.