KPA kufufua uhasama dhidi ya APR vikapu vya Afrika Mashariki

Taifa Leo - - Spoti - NA PHILIP ONYANGO AKIWA DAR ES SALAAM, TANZANIA

VIPUSA wa timu ya mpira wa vikapu Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) wanajitupa uwanjani leo kwa mechi yao ya kwanza ya mashindano ya kanda Afrika Mashariki yaliyong’oa nanga hapa, jana.

Mabingwa watetezi KPA watafungua kampeni dhidi ya APR kutoka Rwanda katika mechi inayotarajiwa kuwa ngumu sana.

Licha ya kupoteza wachezaji wanne muhimu waliosaidia KPA kutwaa taji mwaka jana, kocha Anthony Ojukwu bado anaamini ana uwezo wa kulishinda kwa mwaka wa tatu mfululizo haswa. Imani yake inatokana na KPA kusajili wachezaji watano, ambao wana tajriba kutoka klabu zingine za Kenya na hata ng’ambo.

Wachezaji hao wapya ni Fotso Metemo Helene Michele kutoka Cameroon, Mercy Wanyama na Melisa Akinyi (Storms), Rachael Wandago na Beryl Milungo (Oryx ya Chuo Kikuu cha Kenyatta) na Linet Atieno, ambaye amekuwa akicheza nchini Ushelisheli.

Wale walihamia klabu nyingine ni pamoja na Betty Kananu na Seline Okumu waliotua Equity Bank, Felmas Adhiambo aliyehamia Marekani naye Georgia Adhiambo anachezea A1 Challenge nchini Uganda.

Kenya pia itawakilishwa katika mashindano haya na Equity Bank, ambayo itaanza kampeni yake kesho dhidi ya UCU ya Uganda.

Picha/maktaba Kocha wa kikosi cha Basketiboli cha KPA Sammy Kiki akitoa usia kwa wachezaji wake wakati wa mazoezi kabla ya kuelekea Tanzania kwa michuano ya Afrika Mashariki.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.