Real, Barcelona waambulia sare La Liga

Taifa Leo - - Spoti - MADRID, UHISPANIA

MIAMBA wa soka ya Uhispania, Real Madrid walishindwa kusajili ushindi katika mchuano wa pili mfululizo na hivyo kupoteza fursa ya kutwaa uongozi wa jedwali la La Liga baada ya kulazimishiwa sare tasa na Atletico Madrid ugani Santiago Bernabeu mnamo Jumamosi.

Real ambao walikomolewa 3-0 na Sevilla mnamo Jumatano iliyopita, wangalichupa hadi kileleni mwa msimamo wa jedwali la La Liga kwa kuwapita Barcelona ambao awali walikuwa wamelazimishiwa sare ya 1-1 na Athletic Bilbao katika mchuano mwingine wa Jumamosi.

Fowadi mahiri mzawa wa Wales, Gareth Bale nusura awafungie bao Real kabla ya kuondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha kwanza kutokana na jeraha.

Nafasi maridhawa zaidi kwa Atletico kutikisa nyavu za wenyeji wao ilijiri mwanzoni mwa kipindi cha pili ila juhudi za mvamizi matata mzawa wa Ufaransa, Antoine Griezmann zilizmbulia pakavu baada ya kombora lake kupanguliwa na kipa wa zamani wa Chelsea, Thibaut Courtois.

Mvamizi wa Uhispania, Diego Costa Kiungo wa Real, Luka Modric abanwa na wachezaji wa Atletico katika mechi ya La Liga iliyosakatwa ugani Santiago Bernabeu mnamo Septemba 29, 2018.

hakudhihirisha kabisa makali yake katika mechi hiyo na hivyo kuendeleza ukame wa mabao kapuni mwake katika jumla ya michuano 16 iliyopita ligini.

Ingawa Real walirejelea kampeni za kipindi cha pili kwa matao ya juu, jitihada za wasogora wao zilizimwa na kipa

Jan Oblak ambaye aliwanyima Marco Asensio na Dani Carvajal nafasi nyingi za wazi.

Wakipania kudhihirisha kiwango cha kukerwa kwao na utepetevu wa baadhi ya wachezaji, mashabiki wa Real walianza kuimba jina la Ronaldo ambaye aliagana nao msimu huu na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Juventus.

Real wataendeleza kamepni za kutetea kwa mafanikio ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne watakaposhuka dimbani kupepetana na CSKA Moscow nchini Urusi. Atletico ambao walitawazwa mabingwa wa Ligi ya Uropa msimu jana, watamenyana na Club Brugge ya Ubelgiji siku moja baadaye.

Safari ya Barcelona ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga ilipigwa breki kwa mara nyingine mnamo Jumamosi baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 katika mchuano ulioendeleza msururu wa mechi tatu bila ya kusajili ushindi.

Bilbao ambao walikuwa wageni wa Barcelona, walijiweka kifua mbele kupitia kwa Oscar de Marcos aliyekamilisha kwa ustadi krosi ya Markel Susaeta. Nyota Lionel Messi alitoka benchi katika kipindi cha pili na kushuhudia makombora yake mawili yakibusu mlingoti wa Bilbao.

Alikuwa ni Munir El Haddadi ndiye aliyetokea benchi mwishoni mwa kipindi cha pili na kusawazishia Barcelona baada ya kushirikiana vilivyo na Messi. Makombora ya Philippe Coutinho na Luis Suarez pia yaligonga mwamba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.