Sarri aitaka Chelsea kutolegea kampeni za EPL zikiwaka moto

Mkufunzi huyo amekiri kuwa sare dhidi ya Liverpool ni ishara ya uthabiti wa kikosi chake

Taifa Leo - - Spoti - LONDON, UINGEREZA

KOCHA Maurizio Sarri wa Chelsea amesema kikosi chake kina uwezo wa kuduwaza wengi msimu huu na kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya EPL baada ya kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool wikendi iliyopita na hivyo kuendeleza rekodi ya kutoshindwa muhula huu.

Sarri ambaye ni mzawa wa Italia, aliteuliwa kudhibiti mikoba ya Chelsea mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana rasmi na Napoli aliowaongoza kutinga nafasi ya pili nyuma ya Juventus kwenye kipute cha kuwania ufalme wa Ligi Kuu ya Serie A.

Licha ya mwanzo bora unaojivuniwa na Chelsea katika kivumbi cha EPL hadi kufikia sasa, Sarri anahisi kwamba kikosi chake huenda kikahitaji msimu mmoja zaidi chini yake ili kiweze kutoa ushindani mkali zaidi kwa Liverpool na Manchester City.

Ingawa anakiri kuwa Ligi ya Uingereza ina angalau vikosi sita au saba mahiri na vyenye uwezo wa kutisha mpinzani yeyote katika soka ya bara Ulaya, Sarri anasisitiza kwamba Liverpool na Mancity ndio washindani wawili kwa sasa wanaomkosesha usingizi.

Hata hivyo, anaamini kwamba vijana wake hawajaachwa nyuma kabisa na miamba hao wa soka ya EPL kwa sasa hasa ikizingatiwa udogo wa pengo la alama zinazowatenganisha.

"Kinyume na nilivyokuwa nikifikiria, Chelsea wangali unyo kwa unyo na Liverpool baada ya kuambulia sare katika mchuano uliopita wa EPL uwanjani Stamford Bridge. Ni hatua moja pekee iliyosalia ili tuwafikie viongozi wa jedwali. Naamini hakuna lolote lisilowezekana," akasema Sarri.

Baada ya kuwabamiza Liverpool 2-1 katika mchuano uliowashuhudia wakiwabandua vijana wa Klopp kwenye kipute cha kuwania ubingwa wa Carabao Cup msimu huu, Chelsea kwa sasa wanajivunia kupiga jumla ya michuano miwili bila ya kupoteza hata moja dhidi ya Liverpool ambao wamekutana nao mara

mbili chini ya siku nne.

Chelsea kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 17, mbili nyuma ya Man-city ambao wanaorodheshwa mbele ya Liverpool kutokana na wingi wa mabao wanaoyajivunia kapuni mwao.

"Kuna timu sita au saba hivi katika

EPL ambazo ni miongoni mwa bora katika soka ya bara Ulaya. Kwa muda mfupi ambao nimehudumu uwanjani Stamford Bridge, nimetambua kuwa ni vigumu sana kwa kikosi chochote kutinga mduara wa nne-bora kirahisi na hivyo kufuzu kwa kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA)," akasema Sarri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.