MIAMBA

Taifa Leo - - Spoti - NA GEOFFREY ANENE

MIAMBA Gor Mahia walitawazwa rasmi mabingwa wa Ligi Kuu ya Sportpesa kwa mara ya 17 baada ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Mathare United mjini Kisumu hapo jana.

Walitunukiwa zawadi ya washindi ya Sh4.5 milioni kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya bahati nasibu ya Sportpesa.

Hapo jana, Gor ya kocha Dylan Kerr ilionekana itamaliza ukame wa mechi tatu bila ushindi ilipoongoza mabingwa wa mwaka 2008 Mathare kupitia kwa mabao ya Jacques Tuyisenge na Humphrey Mieno uwanjani Moi. Bao la Tuyisenge ni lake la 14 ligini msimu huu. Linamweka katika nafasi nzuri ya kuibuka mfungaji bora. Aliacha safu ya ulinzi ya Mathare ikidhani ameotea kabla ya kuchenga kipa Job Ochieng’ na kufuma wavuni bao rahisi.

Mieno alifanya mambo kuwa 2-0 dakika ya 53 Mathare ilipozembea kuondoa hatari ndani ya kisanduku chake. Mathare ilipata nafasi kadhaa zikiwemo kutoka kwa Cli Nyakeya, Cli ord Alwanga na James Situma, lakini kipa Peter Odhiambio alikuwa macho michumani na kuzima hatari zote.

Gor ilizembea na kuruhusu Mathare kurejesha magoli yote mawili. Klinsman Omulanga, ambaye alijaza nafasi ya Alwanga dakika ya 50, alifungia Mathare dakika ya 67. Vijana wa kocha Francis Kimanzi walisawazisha 2-2 dakika ya 80 kupitia kwa penalti ya Nyakeya baada ya beki wa Gor, Joash Onyango kuangusha Omulanga ndani ya kisanduku.

Katika mechi nyingine za raundi ya 33 zilizosakatwa jana, AFC Leopards ilikubali kichapo cha tatu mfululizo baada ya kulimwa 2-1 na wageni wao Ulinzi Stars mjini Mumias.

Nayo Sony Sugar ilijihakikishia msimu mwingine kwenye Ligi Kuu baada ya kupepeta Posta Rangers 2-0. Kichapo kilisukuma Rangers karibu na eneo hatari. Iwapo Chemelil Sugar itabwaga Kakamega Homeboyz leo, basi Rangers itakuwa mashakani.

Nzoia Sugar pia ilihatarisha kampeni yake ya kusalia Ligi Kuu baada ya kuchapwa 2-0 na Tusker. Zoo Kericho inahitaji alama moja kutokana na mechi zake mbili zilizosalia kuwa salama kwenye Ligi Kuu. Ilichabanga Thika United 2-1. Thika ilitemwa juma lililopita kwa kuvuta mkia. Vihiga United ilipigana kiume kupata alama moja muhimu katika sare ya 3-3 dhidi ya Kariobangi Sharks na kujiongezea matumaini ya kuepuka shoka. Mechi yake ya mwisho dhidi ya Nakumatt mnamo Oktoba 7 itakuwa kama fainali. Ikishinda Nakumatt ama ipate sare, itasalia katika Ligi Kuu. Nakumatt ilikazana na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Sofapaka hapo jana. Wazito, ambayo imeshaaga Ligi Kuu, ilizima nambari mbili Bandari 2-1 uwanjani Camp Toyoyo.

Kwingineko, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa alijiondoa katika kura za kuchagua mwakilishi wa mwisho wa Bara Afrika kutoka mataifa yanayozungumza Kiingereza kwenye Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zilizofanyika mjini Sharm El Sheikh nchini Misri, jana.

Katika uchaguzi huo wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya Mghana Kwesi Nyatakyi kujiuzulu kutokana na madai alihusika katika ufisadi, Mmalawi Walter Nyamilandu aliibuka mshindi kwa kura 35-14 dhidi ya Danny Jordaan kutoka Afrika Kusini katika raundi ya pili. Raundi ya kwanza ilishuhudia Nyamilandu, Jordan na Mtanzania Leodegar Tanga wakishindwa kupata asilimia 50 ya kura baada ya kuzoa kura 23, 16 na 14, mtawalia. Tenga alijiondoa katika raundi ya pili. Kura hii ya kujaza kiti cha mwanachama wa mwisho (28) katika Baraza la Fifa ilivutia wawaniaji watano, huku Mwendwa na raia wa Ushelisheli Elvis Chetty wakijiondoa mapema jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.