Nitasukuma Mwilu jela, aapa wakili kutoka Uingereza

Bw Qureshi kutoka Uingereza asema ana tajriba ya kimaiatia kufanikisha kazi yake

Taifa Leo - - Front Page - NA MWANDISHI WETU

WAKILI kutoka Uingereza Khawar Qureshi ambaye aliteuliwa kuendesha kesi dhidi ya Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu jana alisema kuwa atahakikisha kuwa Bi Mwilu ametupwa jela.

Bw Qureshi ambaye aliteuliwa na Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Jumatano kuongoza mashtaka katika kesi ya ufisadi dhidi ya Jaji Mwilu alisema kuwa ana weledi unaohitajika kutetea kesi hiyo ya hadhi ya juu.

Mnamo Alhamisi, wakili huyo aliwasili kortini kuanza kazi aliyopewa, lakini mawakili wa Bi Mwilu wakiongozwa na seneta James Orengo, Okong’o Omogeni na Nelson Havi wakaibua pingamizi

Bw Orengo alisema kuwa DPP hana mamlaka ya kuajiri wakili kutoka Uingereza kumwakilisha.

Lakini katika mahojiano na runinga ya Citizan Alhamisi, Bw Qureshi alisema kuwa amefurahia makabiliano kutoka kwa mawakili hao na kwamba yuko tayari kuendeleza kesi hiyo.

“Mimi ni wakili wa kimataifa ambaye amekabiliana na changamoto za maamuzi ya serikali ya UK na mataifa tofauti na kesi kuu za ufisadi ikiwemo Nigeria, Urusi na mataifa mengine ya Afrika ambayo siwezi kutaja. Natumai nitaweza kufahamisha kuhusu masuala hayo,” akasema.

Bi Mwilu anapigana kuzuia kushtakiwa kwake kwa matumizi mabaya ya ofisi, kukosa kulipa ushuru, kupokea Sh12 milioni kutoka benki ya Imperial kwa njia isiyofaa na kupokea mkopo kwa kutumia hila.

Kesi hiyo inasikizwa na majaji Hellen Omondi, Mumbi Ngugi, Chacha Mwita, Francis Tuiyot na William Musyoka.

“Nilielewa kuwa changamoto kwa DPP kushtaki kesi hii ilikuwa kukosekana kwa uwazi na haki lakini anafanya kila awezalo kuonyesha kuwa kuna haki na uwazi kwa kuteua wakili kutoka Uingereza. Huenda hilo litatosheleza,” Bw Qureshi akasema.

“Nimewakilisha serikali nyingi za dunia na ya Uingereza kwa mamia ya kesi ambayo ni ya umuhimu kwa umma,” akasema.

Picha/dennis Onsongo

Wakili wa kimataifa Khawar Qureshi akiwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi, Alhamisi, wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomhusu Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.