Seneta atupwa jela miaka miwili kavu kuhusiana na deni

Mwanasiasa huyo alikosa kutii maelewano ya mashtaka yaliyomtaka arejesha pesa hizo

Taifa Leo - - Front Page - NA SAM KIPLAGAT

ALIYEKUWA seneta maalumu Joy Adhiambo Gwendo, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.7 milioni kutoka kwa shirika moja kaunti ya Kisumu. Hakimu Mkuu Douglas Ogoti jana alisema Bi Gwendo alikuwa mtu asiyeaminika, haswa baada ya kukosa kutii maelewano ya kujibu mashtaka ambayo yalimtaka kurejesha pesa hizo kama njia moja ya kusuluhisha kesi hiyo.

ALIYEKUWA seneta maalum Joy Adhiambo Gwendo, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.7 milioni kutoka kwa shirika moja Kaunti ya Kisumu.

Hakimu Mkuu Douglas Ogoti jana alisema Bi Gwendo alikuwa mtu asiyeaminika, haswa baada ya kukosa kutii maelewano ya kujibu mashtaka ambayo yalimtaka kurejesha pesa hizo kama njia moja ya kusuluhisha kesi hiyo.

Upande wa mashtaka tayari ulikuwa umekubali kumwondolea mashtaka mawili ya wizi na kutengeneza nakala feki.

Lakini akijitetea baada ya kupatikana na hatia, Bi Gwendo alisema kuwa amejutia na kuwa yuko tayari kurejesha pesa hizo, japo mahakama iliendelea kumtupa jela kwa miaka miwili kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi na miezi sita kwa makosa ya kutengeneza cheki feki na kuzipeana.

Seneta huyo wa zamani wa chama cha TNA, alikiri mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi na kupeana cheki feki mbeleni, lakini wakaelewana na upande wa mashtaka kuwa arejeshe pesa hizo kwa kulipa Sh432,930 mara nne.

Shtaka la kwanza dhidi yake lilisema kuwa mnamo Oktoba 23, 2016 eneo la Kisumu Mashariki aliiba Sh2,226,880 za shirika la Kisumu East Cotton Growers Co-operative Scociety.

Korti aidha ilielezwa kuwa mshtakiwa alitengeneza cheki feki cha Sh200,000 kilichonuiwa kutumiwa benki ya KCB na kuipa kwa jina la Kivuli Development Initiative.

Mashtaka mengine yalikuwa kuwa alipeana cheki feki za Sh300,000 na Sh950,000.

Shtaka lingine ambalo mwanasiasa huyo alikataa ni kuwa alitumia nafasi yake kama afisa wa umma kupeana Sh2 milioni kwa shirika hilo, shtaka alilodaiwa kutenda mnamo Oktoba 23, 2016 katika eneo la Chiga, Kaunti ya Kisumu.

Jana, Bi Gwendo alikiri kutoa cheki hizo feki kwa shirika la Kisumu East Cotton Growers Cooperative Society.

Bi Gwendo alishtakiwa mnamo Februari, ambapo alipinga mashtaka hayo matano na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu.

Picha/ Evans Habil

Aliyekuwa seneta maalumu Joy Adhiambo Gwendo akiwa katika mahakama ya Alhamisi ambapo alishtakiwa kupeana cheki katika jumba la mikutano la KICC, Nairobi mwaka wa 2016 akijua akaunti iliyolengwa haikuwa na pesa za kutosha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.