Nzili, wakuu wa NHIF kushtakiwa kwa sakata ya Sh1.1b

Taifa Leo - - News - NA CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mkurungenzi Mkuu Mtendaji wa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu (NHIF) Simeon Kirgotty jana alikamatwa kuhusiana na sakata ya wizi wa Sh1.1 bilioni kupitia mpango wa ununuzi wa mfumo wa ukusanyaji mapato kidijitali.

Bw Kirgotty alikamatwa na maafisa wa upelelezi mjini Nairobi pamoja na msimamizi wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Gilbert Gathuo na afisa mkuu wa kampuni ya Web Tribe maarufu kama Jambo Pay.

Watatu hao walipelekwa katika kituo cha Polisi cha Muthaiga kabla ya kuhamishwa hadi Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) yanayopatikana katika barabara ya Kiambu kuhojiwa.

Duru zilisema kuwa watatu hao watahitaji kutoa maelezo kuhusu matumizi mabaya ya pesa za umma kuhusiana na uagizaji wa mitambo kufanikisha malipo kidijitali.

Uchunguzi ulibaini kuwa usimamizi wa NHIF chini ya Bw Kirgotty mnamo 2014 ulitoa zabuni kwa mfumo huo wa malipo kwa Jambo Pay bila kufuata sheria ya ununuzi wa bidhaa za umma.

Malipo

Kufikia Agosti mwaka huu, shirika la NHIF lilikuwa limetumia zaidi ya Sh1 bilioni kupitia mpango huo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alisema kwamba maafisa wengine 21 watafunguliwa mashtaka kuhusiana na sakata hiyo akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha Walimu, Knut Bw Mudzo Nzili.

Wiki hii NHIF ilimtuma Afisa Mkuu Mtendji Geoffrey Mwangi kwa likizo ya lazima siku moja baada ya kukamatwa kwa kosa la kuzuia uchunguzi kuhusu kesi ya ufisadi. Bw Mwangi pamoja na Mkurugenzi wa Fedha Joseph Mbuvi walidaiwa kudinda kuwasilisha stakabadhi zilizohitajika na wapelelezi wa EACC katika uchunguzi wa sakata ya kupotea kwa Sh100 milioni.

Wawili hao walifikishwa mahakamani Nairobi Jumatano lakini wakaachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.