Bunduki nyingi ndio zinaongeza wizi, wazee walalamika

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA OSCAR KAKAI

WAZEE kutoka Kaunti ya Pokot Magharibi wamelalamikia kukithiri kwa visa vya wizi wa ng’ombe na ujangili katika mipaka ya kaunti hiyo na jirani zake kutokana na kuwepo kwa bunduki nyingi mikononi mwa jamii za wafugaji.

Mamia ya wenyeji wamefariki baada ya kupigwa risasi na majangili na mifugo kuibwa huku ikibainika zaidi ya bunduki 50,000 zipo mikononi mwa jamii za wafugaji zinazoishi Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya usalama, jamii za wafugaji zimekuwa zikijihami kwa bunduki kwa miaka mingi kutokana na uhasama ulioota mizizi kati yao na kushindwa kwa serikali zilizopita na ya sasa kuwapa ulinzi dhidi ya uvamizi wa mahasimu.

Kando na wafugaji, wataalam hao wanasema kwamba bundiki kati ya 530,000 na 680,000 zinamilikiwa na watu mbalimbali kitaifa. Jamii za Pokot, Turkana, Marakwet, Tugen, Samburu na Injemus ndizo zinamiliki idadi kubwa za bunduki.

Kulingana na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Pokot John Muok, jamii hiyo ilianza kununua bunduki nchini Uganda wakati utawala wa Dikteta Idi Amin Dada ulipopinduliwa na Rais wa zamani Milton Obote mwaka 1971.

Baada ya mapinduzi hayo, bunduki ziliendelea kuingizwa hapa nchini kwa kishindo hadi ikafikia kiwango ambacho serikali haingeweza kudhibiti kuingizwa kwa silaha hizo.

“Miaka 40 iliyopita wakazi wa Pokot Magharibi walishiriki vita vikali na jamii jirani wakitumia silaha za kawaida kama mikuki na mishale. Baada ya uhuru, jamii za Pokot na Karamojong zilipigana vita vikali na kuongezeka kwa visa vya ujangili," asema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.