Kanisa lataka adhabu ya ufisadi ijumuishe kunyongwa

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA ERICK WAINAINA

KANISA sasa linataka makali ya sheria zilizotungwa za kupigana na ufisadi yaongezwe zaidi ili kuhusisha adhabu ya kunyongwa kwa maafisa wanaoshikilia nyadhifa kwenye ofisi za umma wanaoshiriki ufisadi.

Baraza Kuu la Kitaifa la Makanisa nchini kupitia Kasisi Peter Karanja aliyesoma taarifa yao jana kwenye Jumba la Jumuiya mjini Limuru linataka adhabu hiyo ijumuishwe kwenye sheria za kumaliza ufujaji wa mali ya umma.

Viongozi wa makanisa hata hivyo walisisitiza kwamba maafisa wa umma wanaokubali walishiriki ufisadi wanafaa kusamehewa baada ya kulazimishwa kurejesha mali waliyoiba.

“Mzaha na maneno matupu kwa wafisadi sasa unafaa kupisha uamuzi wa kitaifa usiopingika wa kuwakabili wafisadi,” akasema Kasisi huyo.

Baraza hilo lililoandaa warsha ya siku mbili mjini Limuru kushughulikia maswala ya kanisa na mambo yanayoathiri taifa pia lilitaka ufisadi utajwe kama janga la kitaifa kwa kuwa umechangia matatizo chungu nzima yanayokumba nchi.

“Kenya huenda ikapoteza zaidi ya Sh700 bilioni mwaka huu pekee iwapo madai ya serikali ni kweli. Hakuna taifa linaloweza kuhimili kiasi hicho cha ubadhirifu na wizi,” akasisitiza Bw Karanja.

Baraza hilo vile vile lililaumu serikali kwa kukopa pesa kiholela kutoka mataifa ya nje.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.