Mlinzi wa chuo kikuu akamatwa kuhusu mauaji ya mjombake

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - Na Tabitha Onyango

BAWABU mmoja katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga, jana alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mwalimu wa shule ya msingi eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya.

Mshukiwa huyo alikamatwa baada ya mwalimu huyo, ambaye pia ni mjomba wake kudhibitishwa kufa katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga ambapo alikuwa akitibiwa.

Marehemu, Bw Johannes Otieno, mwalimu wa Shule ya Masita, alivamiwa Jumanne asubuhi katika kijiji cha Usoko na kuuawa.

Chifu wa eneo hilo Walter Omollo alisema kuwa wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja, baada ya mkewe marehemu kuondoka walipokosana na mumewe.

“Bado hatujabaini kilichotokea kwani mshukiwa na marehemu walikuwa wawili tu wakati kisa hiki kilitokea,” akasema Bw Omollo.

Mshukiwa anasemekana kukimbia kuripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Bondo baada ya kugundua kuwa mjomba wake alikuwa ameanguka na hakuwa akifanya lolote, lakini baadaye akakamatwa na kurejeshwa humo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.