MCAS wagawika katika mpango wa kuvunja bunge

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA MWANDISHI WETU

WAWAKILISHI wa wadi katika Kaunti ya Homa Bay wamegawanyika kuhusiana na mpango wa kuvunjilia mbali bunge la kaunti hiyo.

Wawakilishi hao walitofautiana kuhusu majaribio ya kuitisha uchaguzi mpya kama jambo la kimkakati kuzima moto ndani ya bunge hilo linaloendelea kushuhudia mizozo ya uongozi.

Upande mmoja wa karibu wanachama 20 ukiongozwa na Bi Joan Ogada na mratibu wa wengi Bungeni Bw Richard Ogindo wamedokeza kuwa huenda wakajiuzulu wiki ijayo.

Wengine wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni Bw Walter Muok walisema kuwa hawataachilia nyadhifa zao.

Hao ni pamoja na wawakilishi 35 ambao wamekataa kumtambua Spika Elizabeth Ayoo kama Kiongozi wa Bunge hilo.

Spika huyo kwa sasa anahudumu chini ya agizo la muda. Baadhi ya wanachama ambao wametishia kujiuzulu ni Bi Ruth Ombura, Bi Lorna Owino, Bi Jane Kiche, Bi Sophie Koweje, Bi Mary Gaya, Bi Esther Dualo miongoni mwa wengine.

Bw Muok alisema kujiuzulu kwake hakutaathiri operesheni katika bunge hilo.

“Kundi la wawakilishi wanaotishia kujiuzulu lina karibu wawakilishi watano ambao walichaguliwa na wananchi. Kutokuwepo kwao hakutatuzuia kutotekeleza majukumu yetu kwa sababu tutakuwa tumetosha. Nafasi za wawakilishi maalum zitapeanwa mara moja na ODM wakijiuzulu,” alisema Bw Muok.

Kiongozi huyo wa wengi alisema Bunge hilo linajihusisha na shughuli kadhaa, miongoni mwake, mjadala kuhusu miswada minne ikiwemo ule wa fedha, elimu na ufadhili wa elimu na ugamvi wa rasilimali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.