RAIS AJA NA MINOFU NYANZA -RAILA

Kinara wa upinzani ahimiza wakazi kujitokeza kwa wingi kumlaki rais kwa bashasha wiki ijayo

Taifa Leo - - Front Page -

VICTOR RABALLA NA CAROLINE MUNDU KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga amewadokezea wafuasi wake kuwa Rais Uhuru Kenyatta atawaletea mapochopocho wakati wa ziara yake mjini Kisumu wiki ijayo atakapokuja kuzindua Mpango wa Afya kwa Wote (UHC).

Huku akiwahimiza kumlaki Rais Kenyatta kwa furaha na bashasha, kiongozi huyo wa ODM alisema ushirikiano wao tayari umeanza kuzaa matunda kufuata utulivu ambao unaoshuhudiwa nchini.

“Tunajua mahala ambako tunataka kwenda na ninawahakikishia kuwa mengi mazuri ya yanakuja kwa sababu tumeanza mpango wa kupalilia amani na kuhakikisha kuwa Wakenya wanadumisha umoja,” akasema jana wakati wa mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Posta, Kisumu.

Bw Odinga alieleza imani yake kwamba, muafaka kati yake na Rais Kenyatta utarejesha taifa katika hali ya upendo miongoni mwa Wakenya jinsi ilivyokuwa Kenya ilipopata uhuru.

“Nakumbuka nikiwa mtoto, Rais wa kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta angelala nyumbani kwetu mara kadha. Tunapaswa kulirejesha taifa hili katika enzi hizo ambapo wananchi waliungana na hawakugawanywa na ukabila.

Bw Odinga alisema muafaka huo utakomesha ghasia ambazo hutokea kila baada ya uchaguzi mkuu.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuwasili Kisumu Alhamisi wiki ijayo kuzindua mpango huo wa afya kwa wote ambao utagharimu Sh800 milioni. Waziri wa Afya katika serikali ya kaunti ya Kisumu Rosemary Ombara alisema zaidi ya watu 23,000 wamesajiliwa kwa mpango huo ambao unalenga kuwafaidi watu 240,000

Akiwahutubia wanahabari afisini mwake jana, Dkt Ombara alisema Sh435 milioni zitatumika kuwaajiri wahudumu wapya, Sh132 milioni kuwaajiri wahudumu wa afya ya kijamii huku Sh40 milioni zikitumiwa kununua vifaa vya kuwapima wagonjwa.

“Tunafahamu kuwa hospitali zetu zinakabiliwa na uhaba wa wahudumu, vitanda na hata ambulansi ya kuwasafirisha wagonjwa mahututi. Hata hivyo, mahitaji haya yote yamejumuishwa katika bajeti ya ziada,” akasema.

Kaunti ya Kisumu ni moja kati ya kaunti nne zilizoteuliwa kuendesha majaribio ya mpango huo wa UHC kutokana na hali kwamba hukumbwa na visa vingi vya mkurupuko wa magonjwa ya kuambukizwa.

Kaunti zingine ambako mpango huo utazinduliwa ni Nyeri, Kitui na Machakos.

Gavana wa Kisumu ambaye alihutubu wakati wa mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Posta aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais atakapokuwa akizindua mpango huo wa kihistoria.

“Endapo kuna tofauti zozote baini yetu, huu ni wakati wa kuziweka kando na kumualika mgeni wetu kwa furaha na ambaye bila shaka atatuletea mazuri,” akasema.

Viongozi wengine walioapa kumkaribisha Rais Kenyatta mjini Kisumu ni pamoja na naibu Gavana Mathews Owili, Seneta Fred Outa na Mbunge wa Kisumu ya Kati Fred Ouda.

Picha/ondari Ogega

Kiongozi wa ODM Raila Odinga ahutubia wafuasi wake nje ya a si za chama hicho katika uwanja wa Posta, Kisumu jana. Bw Odinga alihimiza wakazi wa sehemu hiyo kujitokeza kwa wingi kumlaki rais wiki ijayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.