Vita vya ufisadi visilenge eneo fulani-ruto

Ataka korti kutoa maamuzi kwa misingi ya sheria, uwazi

Taifa Leo - - News - NA DENNIS LUBANGA

NAIBU wa Rais William Ruto jana alitoa matamshi makali dhidi ya mamlaka za kupigana na ufisadi akisema zinaegemea maeneo fulani na kuingiza siasa ndani ya vita hivyo, siku chache tu baada viongozi kutoka eneo la Bonde la Ufa kudai vita hivyo vinalenga watu wa jamii ya Kalenjin. Akizungumza katika kaunti ya Elgeyo Marakwet jana, Bw Ruto alidai mamlaka za EACC, DCI, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na idara ya mahakama hazijafanya kazi yake ipasavyo akizitaka kuhudumu inavyofaa. “Viongozi wa mashtaka na wachunguzi hawafai kuingiza siasa kazini kwani jukumu lao ni wazi. Kwa hivyo tusiingize siasa kwa mashirika ya kuendesha mashtaka. Yaachwe yafanye kazi kwa uwazi, bila kuegemea siasa ama maeneo fulani,” Bw Ruto akasema.

“Mahakama aidha ziachwe zifanye maamuzi kwa misingi ya sheria na haki ili zisiangushe demokrasia ya taifa na namna umma unahudumiwa,” akasema.

Naibu wa Rais alikuwa akizungumza katika shule ya Lelboinet, kaunti ya Elgeyo Maralkwet ambapo aliandamana na viongozoi wa eneo la Bonde la Ufa wakiwemo Magavana Jackson Mandago (Uasin Gishu), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), wabunge, Daniel Rono (Keiyo Kusini) na Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini).

Lakini matamshi haya ya Bw Ruto yalitokea siku chache tu baada ya viongozi kutoka Bonde la Ufa kulalamika kuwa vita dhidi ya ufisadi vimekuwa vikilenga maafisa wa serikali wanaotoka katika jamii, kwa lengo la kuwafuta kazi.

Viongozi hao walichemka baada ya Meneja Mkurugenzi wa Kenya Pipeline Joe Sang kujiuzulu katika kile kilionekana kama kufutwa kazi na serikali, kuhusiana na kesi dhidi ya ufisadi.

Viongozi hao walidai kuwa japo naibu wa Rais alikuwa ametengewa nafasi asilimia 50 serikalini baada ya uchaguzi wa 2013, kwa sasa hali inazidi kubadilika viongozi wa eneo hilo wakitafutiwa makosa na kupigwa kalamu, huku naye Bw Ruto akipakwa tope kuwa ni mfisadi ili kuhujumu mbio zake za ikulu za 2022.

“Kwa kipindi cha chini ya miezi sita, Maafisa Wakuu Watendaji (CEOS) wamefutwa kazi kutoka jamii moja. Ni kosa gani tumefanya? Kama jamii tuna hofu kwani kuna watu, kwa sababu tusizojua, wanataka kuwang’atua maafisa wa jamii ya Kalenjin kutoka ofisini, ilhali wamehitimu vizuri,” akasema mbunge wa Aldai Cornelius Serem.

Lakini Rais Kenyatta amezidi kushikilia kuwa hakuna kurudi nyuma katika vita dhidi ya ufisadi, akirejelea hayo Jumatano alipokuwa Kiambu.

Baadhi ya maafisa waliopigwa kalamu kutoka jamii hiyo ni aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta Lilly Koros, waliokuwa mameneja wakurugenzi wa Kenya Power Ben Chumo na Ken Tarus, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa bodi ya NCPB Newton Terer na wa hivi punde zaidi, Bw Joe Sang.

“Kila uchao inakuwa wazi kuwa hivi vita dhidi ya ufisadi vinalenga eneo moja, mambo hayafanywi inavyofaa,” akasema mbunge wa Belgut Nelson Koech.

Picha/jared Nyataya

Naibu Rais W William Ruto (kati), Mbunge wa Kitutu Chache Richard Onyonka (kushoto), na Mbunge wa Keiyo South Daniel Rono wakati wa harambee eneo la Lelboinet, Keiyo South jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.