Kenya bado nyuma katika kuangamiza TB, shirika ladai

Shirika la Afya Duniani lasema Kenya imesalia katika mataifa 30 ambayo yamelemewa

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA FRANCIS MUREITHI

KENYA bado haijapiga hatua kupunguza visa vya ugonjwa wa kifua kikuu huku visa 85,188 pekee vikiripotiwa kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) mwaka jana.

Hivyo, inamaanisha mwaka huu unapokaribia tamati Kenya itasalia katika orodha ya mataifa 30 ambayo bado yanalemewa na ugonjwa huo kote duniani.

Kulingana na WHO, Kenya inafaa kulifahamisha shirika hilo kuhusu visa 169,000 vya wagonjwa wa TB wasiojulikana.

Wataalamu wa afya wameonya kuhusu hatua hiyo ya kukosa kuwasilisha ripoti za TB, wakisema wagonjwa wowote ambao hawajatambuliwa na kutibiwa ni hatari kwa jamii kwani mmoja anatosha kuambukiza watu 10-15.

Kifua kikuu kinashikilia nafasi ya nne katika orodha ya magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo nchini.

Inakisiwa takriban watu 140,000 huambukizwa maradhi hayo kila mwaka.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa, jinsi visa vingi zaidi vya TB vinavyoripotiwa na wagonjwa kupewa matibabu ndivyo kiwango cha maambukizi kinapungua.

Maafisa wanaohusika na TB katika Wizara ya Afya wanasema kuwa nusu ya visa vya ugonjwa huo hatari havijatambuliwa.

“Kwa sababu tumekosa kutimiza shabaha kwa karibu asilimia 50 inamaanisha TB ingali imeenea miongoni mwa watu wanaotafuta matibabu hospitalini,” alisema Mkuu wa Matibabu ya TB katika Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu, Dkt Stephen Muleshe.

Hata hivyo, Dkt Muleshe alisema serikali imeimarisha juhudi kuhakikisha visa hivyo vya TB ambavyo havijaripotiwa, vinafanywa hivyo.

“Kwa sasa tunatekeleza mpango wa kusaka visa vyovyote, Active Case Findingi, ambapo wagonjwa wote hupimwa kubaini iwapo wameambukizwa kifua kikuu,” aliongeza.

Alikuwa akizungumza Alhamisi mjini Nakuru wakati wa kikao na wanahabari kujadili mbinu bora zaidi za kuandaa habari za ugonjwa huo.

Mkuu huyo wa matibabu ya TB alisema ishara za maambukizi ni pamoja na kikohozi kisichokoma, joto la mwili, kutokwa na jasho usiku, kupungua kilo, uchungu kifuani, damu katika kikohozi na kukosa hamu ya chakula.

Takwimu zinaonyesha kuwa vifo vinavyotokana na TB vilipungua kutoka 6,414 mwaka 2011 hadi 4,735 mwaka 2016 kutokana na kampeni thabiti ya serikali kutambua visa vyovyote na kuanza tiba mara moja.

Picha/maktaba

Afisa wa matibabu afanya utafiti kuhusu maradhi ya kifua kikuu nchini Afrika Kusini. Kenya imeshutumiwa kwenda mwendo wa kinyonga kukabili maradhi hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.