Wabunge watalipiza kisasi Rais kupinga nyongeza zao?

Huenda miswada, chaguo la majina ya uteuzi serikalini yawe yakiangushwa na wabunge

Taifa Leo - - Front Page - NA CHARLES WASONGA

HUENDA kukatokea hali ya vuta nikuvute kati ya Afisi ya Rais na Bunge mwaka ujao kuhusiana na hatima ya Mswada wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) unaopendekeza wabunge waongeweze marupurupu na manufaa mengineyo.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuapa kwamba kamwe hatatia saini mswada huo ukipitishwa na wabunge kisha kuwasilishwa kwake, akisema utawaongezea wananchi mzigo wa gharama ya maisha.

Msimamo huu wa Rais ulipelekea Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC) kuondoa mswada huo katika ratiba ya shughuli za bunge Alhamisi, siku ambayo ulitarajia kupitia kura na kupitishwa ili uvukishwe katika hatua ya tatu. Ni baada ya awamu hii ambapo mswada huo ungepitishwa kisha kuwasilishiwa Rais Kenyatta auidhinishe kuwa sheria.

Mbunge mmoja wa chama cha Jubilee ambaye aliomba tulibane jina lake alisema wao pia watalazimika kuonyesha makali yao kwa kutopitisha mswada iliyodhaminiwa na serikali au majina ya watu walioependekezwa kushikilia nyadhifa mbalimbali serikalini.

“Tulidhihirishwa uwezo na mamlaka yetu wiki ijayo Desemba 14 wakati Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) itampiga msasa Bw Twalib Abdallah Mbarak aliyependekezwa kwa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC),” akasema mbunge huyo kutoka eneo la Rift Valley.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, hata hivyo, anashikilia kuwa itakuwa vigumu kwa wabunge kuangusha miswada ya serikali au chaguo la rais bungeni.

"Rais ana mbinu nyingi za kuwalazimisha wabunge kutia amri yake ikizingatiwa kuwa baadhi yao wanazongwa na mizigo ya madeni na sakata kadhaa za ufisadi," anasema Bw Andati.

Wabunge tuliwahoji kwa ajili ya makala haya walisema hawakuona haja ya kupigia kura mswada huo baada ya Rais, kiongozi wa upinzani Raila Odinga na wananchi kwa jumla kupotoshwa kwamba unalenga kuwaongezea mishahara.

“Vyombo vya habari viliamua kimakusudi kupotosha umma kuhusu mswada huu kwa kudai unalenga kutuongezea mishahara ilhali huo sio ukweli. Na inasikitisha kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamenaswa na uwongo huu,” akasema kiongozi wa wachache Bw John Mbadi.

“Ndio maana tuliamua kuondoa shughuli ya kupigiwa kura kwa mswada huo katika orodha ya shughuli za leo (Alhamisi). Sio kweli kwamba tuliingizwa baridi na kauli ya rais. Tutaupitisha mswada huu mwaka ujao na kuuwasilisha kwa Rais,” akasema.

Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma vilevile anashikilia uzi huo huo akisema kuwa umma ulipotosha kuhusu dhima ya mswada huo, akisema haupendekezi nyongeza yoyote ya mapato ya wabunge.

“Azma kuu ya mswada huu ni kukita utendakazi wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kwenye Katiba ya Kenya ili kuafiki hitaji la kipengee cha 127 cha Sheria hiyo kuu. Wajibu wa tume hii ni kuhakikisha kuwa wabunge wanapewa misaada faafu kuwawezesha kutekeleza majukumu yao yaliyoorodheshwa katika vipengee vya 94 na 95,” anasema.

“Haupendekezi nyongeza ya mishahara yetu. Wajibu wa kuongeza ua kupunguza mishahara ni wa Tume ya Mishahara (SRC),” anakariri mbunge huyo ambaye ni wakili.

Kimsingi, mswada huo, ambao nakala yake

Taifa Jumapili ilipata, unapendekeza kuwa wabunge wote 349 na maseneta 67 watakuwa wakipokea marupurupu ya usafiri ihali wao hupewa ruzuku ya Sh7 milioni za kununua magari.

Aidha, unapendekeza kuwa wabunge wapewe magari rasmi yenye nambari za usajili za GK, sawa na mawaziri na makatibu wa wizara. Hii bila shaka itamaanisha kuwa bajeti ya Bunge itapanda kuzidi ilivyo sasa, mzigo ambao utabebeshwa mlipa ushuru.

Vilevile, mswada huo kwa jina “Parliamentary Commission Service Bill 2018” unapendekwa kwamba wabunge wapewe marupurupu ya nyumba licha ya kwamba wakati huu wao hupewa mkopo wa kununua nyumba wa kima cha Sh20 milioni.

Na ukitiwa saini kuwa sheria, wake wa pili, na wa tatu, wa wabunge wa kiume pia watajumuishwa katika bima ya matibabu yanayolipiwa kwa pesa za umma.

Isitoshe, mswada huo unapendekeza kubuniwa kwa hazina maalum ya kufadhili shughuli ya wabunge ya kukagua miradi ya serikali ya kitaifa katika maeneo bunge wanakowakilisha. Hazina nyingine pia itabuniwa ya kufadhili mpango wa kushirikisha umma katika shughuli za bunge, maarufu kwa kimombo kama, “Public Participation.”

Mtaalamu wa masuala ya uchumi Kwame Owino anasema kutekelezwa kwa mapendekezo hayo, na mengineyo, kutapelekea kupanda kwa bajeti ya bunge ambayo hufadhili kwa mfuko wa umma.

“Ikiwa mswada huo utakaopitishwa na hatimaye kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta, sambamba na mapenzi ya wabunge. Hii ina maana kuwa bajeti ya sasa ya bunge ambayo ni Sh36 bilioni katika mwaka huu wa kifedha itapanda hadi zaidi ya Sh40 bilioni,” anasema.

Na kwa upande wake Bw Odinga aliwasuta wabunge kutokana na mpango wao wa kujiongezea mapato akisema hiyo ni ishara kuwa hawajali masihali ya wananchi.

Saa chache baada ya tamko hilo la Rais kiongozi wa wengi Aden Duale, Alhamisi, alichelea kusema lolote kuhusu mswada huo alipokuwa akitoa maelezo kuhusu miswada ambayo itapewa kipaumbele bunge litakaporejelea vikao vya mwezi Februari, 2019.

Rais Kenyatta aliwataka wabunge kuyapa kipaumbele masuala yenye manufaa kwa Wakenya kwanza badala ya yale yanayowafaidi kama watu binafsi.

“Kama viongozi, hatupaswi kujishughulisha zaidi na masuala ya kujiongezea mapato, bali tunafaa kuyapa kipaumbele mahitaji ya watu wetu,” akaeleza.

Itakumbukwa kwamba katika bunge la 10, wabunge waliweza kujiongeza mishahara hadi kufikia kima cha Sh890,000 bila marupurupu kadhaa. Hii ilimaanisha kuwa waliweza kutia kibindoni zaidi ya Sh1 milioni kila mwezi.

Na licha ya SRC kupunguza mishahara yao hadi Sh530,000 2014, wabunge walitumia vitisho kuhakikisha kuwa wanaendelea kupokea marupurupu kadhaa na ruzuku ya Sh7 milioni za kununua magari.

Maktaba Picha/

Wabunge wakijadili mswada wa Jinsia ndani ya Bunge la Kitaifa mwezi uliopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.