Waziri ahakikishia vyombo vya habari Serikali italipa deni lao

Taifa Leo - - Front Page - ANITA CHEPKOECH na WINNIE ATIENO

SERIKALI imewahakikishia wamiliki wa vyombo vya habari kuwa deni lao litalipwa.

Serikali inadaiwa mabilioni ya pesa na vyombo vya habari kwa kupeperusha matangazo ya mauzo.

Akiongea kwenye warsha ya siku mbili ya wahariri jijini Nairobi, waziri wa mawasiliano na teknolojia Joe Mucheru alisema serikali italipa pesa wanalodaiwa na vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari ni nguzo kuu katika maendeleo ya taifa na tunatambua hilo. Tutalipa deni lenu haraka iwezekano na hata Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiuliza kama tumeshawalipa,” akasema waziri huyo.

Serikali inadaiwa Sh2.5 bilioni kutokana na matangazo ya mauzo (Advertising) katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Bw Mucheru alimhakikishia afisa mkuu wa shirika la habari la Nation Media Group, Bw Stephen Gitagama ambaye alimuuliza waziri huyo kuhusu deni lao.

”Lipeni madeni,” alisisitiza Dkt Gitagama kwenye warsha hiyo katika hoteli ya Villa Rosa Kempinski.

Bw Mucheru alisema wanafanya bidii kulipa deni hilo.

"Najua hilo ni suala tata katika warsha hii lakini tunatia bidii, tunawekwa kwa presha pia sisi,” akasema.

Alisema vyombo vya habari vina uwezo mkubwa na serikali inatambua hilo.

Pia alitaka vyombo vya habari kukumbatia teknolojia ili kukuza uanahabari.

Dkt Gitagama alisisitiza kuwa mkutano huo ni muhimu kujadili changamoto katika sekta ya habari nchini.

"Uanahabari unabadilika kila uchao, kuna hatari zaidi kwenye uhuru wa habari duniani,” alisema Dkt Gitagama.

Lakini aliwataka wanahabari kuheshimu sheria.

Naye Balozi wa Marekani humu nchini Robert Godec alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kukuza waandishi wa habari wa kike.

Picha/ Jeff Angote

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru alipohudhuria warsha ya wahariri jijini Nairobi hapo jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.