Malipo kwa walevi kila siku yagawanya wanasiasa

Taifa Leo - - Front Page - NA ERIC WAINAINA

VIONGOZI katika kaunti ya Kiambu wamegawanyika pakubwa kuhusiana na mradi unaoendeshwa na Gavana Fer-

dinand Waititu wa ‘kuwarekebisha’ walevi na majambazi, kwa kuwalipa Sh400 kila siku.

Viongozi wa kaunti hiyo sasa wanadai Bw Waititu anatumia vijana hao takriban 6,500 kwa manufaa yake ya kisiasa. Walisema huwa wanachochewa kuvuruga mikutano na kuwazomea viongozi wanaopinga mipango yake.

Hali kama hiyo ilijitokeza mbele ya Rais Uhuru Kenyatta Jumatano, wakati Bw Waititu na mwakilishi wa wanawake wa kaunti hiyo Gathoni Wa Muchomba walitofautiana hadharani.

Bi Wa Muchomba aliaibishwa na vijana wanaonufaika na mradi wa Gavana Waititu wa “Kaa Sober”, ambapo kwa jumla huwa wanalipwa takriban Sh2milioni kila siku, kwa madai ya kuwasaidia kujikomboa kutokana na ulevi.

Bi Wa Muchomba na Gavana Waititu wanaendesha miradi tofauti ya kuwarekebisha walevi, lakini wamekuwa wakitofautiana kuhusu mbinu inayofaa huku Bw Waititu akishambuliwa na viongozi wa eneo hilo kuwa anafanya isivyofaa.

Viongozi hao wawili walibishana mbele ya Rais, Bw Waititu akiwa amesafirisha mamia ya vijana hao kwa mabasi hadi uwanja wa Ndumberi.

Viongozi wa Kiambu wanadai vijana hao wamekuwa wakihudhuria mikutano ambapo Gavana Waititu yupo na kuwapigia makelele viongozi wanaoonekana kuwa mahasimu wake.

Viongozi kadha wakiwemo Bi Wa Muchomba, seneta Kimani Wamatangi, mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na seneta maalum Isaac Mwaura wanasemekana kuwa tayari wamepiga ripoti kwa polisi kuwa kikundi hicho kinaweza kuwa genge la kisiasa linalochipuka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.