Raila akemea wabunge akisema wana ubinafsi

Taifa Leo - - News - Na KNA

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amewataja wabunge wabinafsi kwa kupanga kujiongezea mishahara.

Bw Odinga alisema hatua hiyo inafaa kukataliwa kwa vyovyote vile ili kupunguzia nchi mzigo wa gharama kubwa ya mishahara.

Alisema Wakenya wamezidiwa na ushuru na hawawezi kuhimili nyongeza ya mishahara na marupurupu kwa Wabunge.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa hatua hiyo ni kinyume na Katiba na inafaa kukataliwa na Wakenya wote.

Wabunge wanafaa kujua kuwa wamo chini ya sheria. Tuna taasisi ya kikatiba ‘Tume ya Mishahara na Marupurupu’ (SRC) ambayo tayari imeamua mishahara ifaayo kwa wabunge,” alisema mjini Kisumu Ijumaa.

Bw Odinga alisema mishahara zaidi kwa Wabunge ni ufujaji wa mali ya umma. Alisema tamaa hiyo pia imeanza kushuhudiwa katika serikali za kaunti ambapo wawakilishi wa wadi wameonekana kutumia vibaya mali ya umma katika ziara za kupokea mafunzo.

“Kila wakati wanaenda ziara ili kupata marupurupu kwa kudai kuwa wanaenda kusoma. Lazima waambiwe kuwa Wakenya wamechoka,” alisema.

Alionya wabunge kuwa wakiendelea kusukuma kuongezewa mshahara, bila shaka Wakenya watapinga hilo.

Bw Odinga aliwataka Wabunge kulenga kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia, kuwakilisha na kuunda sheria kwa lengo la kuleta mabadiliko nchini.

Raila yumo Kisumu kwa maandalizi ya ziara ya Rais Uhuru Kenyatta jijini humo wiki ijayo kuzindua mpango wa afya kwa wote (UHC).

PICHA/MAKTABA

Bw Odinga akiwa mjini Kisumu, Ijumaa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.