Mlinzi auawa na wezi wa Sh700,000 kituoni cha kuuza mafuta

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA MANASE OTSIALO

MLINZI mmoja aliuawa katika kituo cha kuuza mafuta mjini Mandera Ijumaa na takriban Sh700,000 kuibwa

Kundi la watu saba waliingia katika kituo cha mafuta cha Takbir na kuagiza walinzi wawili wa usiku kulala chini, alisema kamanda wa polisi wa Mandera Mashariki Ezekiel Sing’oe.

Afisa huyo alisema walinzi hao walifungwa mikono na miguu na wavamizi wao ambao walivunja sefu na kuchukua pesa hizo.

Bw Singo’e alisema washambuliaji hao walikuwa wamevaa sare za polisi.

“Tulifahamishwa kwamba wezi hao walikuwa wamevaa sare za polisi,” alisema, na kuongeza kuwa mlinzi huyo aliuawa alipojaribu kupiga mayowe.

“Alipigwa kichwani nyuma kwa kifaa butu,” alisema na kutambulisha mwanamume aliyeuawa kama Dakane Abdille Abdi na mwenzake kama Salat Osman Jelle.

Wezi walivunja milango mitatu ya chuma kabla ya kufikia sefu hiyo.

Aliyeshuhudia kisa hicho na ambaye hakutaka jina lake kuchapishwa alisema washambuliaji hao huenda walijua operesheni katika kituo hicho.

“Ni watu wa kutoka eneo hili, sio watu waliotoka mbali au mji wa Bulahawa (Somali) kwa sababu walijua kilichokuwa kwenye sefu hiyo,” alisema.

Walioshuhudia kisa hicho walisema kilitokea licha ya kuwa eneo hilo huwa na ulinzi mkali sana usiku hasa kutokana na tishio la al-shabaab.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.