Wakadiria hasara baada ya ndovu kuharibu mashamba yao

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA LUCY MKANYIKA

WAKAZI wa Sagalla mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta, wanakadiria hasara kubwa baada ya makundi ya ndovu kuharibu mali na mimea yao.

Eneo hilo huvamiwa mara kwa mara na ndovu ambao huwa wanahama kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Mkomanzi nchini Tanzania kuelekea Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo East.

Inasemekana eneo hilo ni njia inayotumiwa na ndovu wanapofanya safari yao. Jumatano usiku, kundi moja la ndovu lilivamia boma la Nickson Mwangemi mwendo wa saa sita na kuharibu nyumba pamoja na mali yao.

Kulingana na Bw Mwangemi, ndovu mmoja alilenga nyumba yake ya matofali katika kijiji cha Mwakoma wakati mkewe na watoto wao watatu walikuwa wamelala.

Mkewe, Patience Karisa, pamoja na watoto walilazimika kujificha katika kona ya nyumba kumkwepa ndovu huyo.

Bidhaa za nyumba zilitupwa nje na mimea kuharibiwa. Mzee wa kijiji cha Ndara Bw Silas Mwambiji alisema wakazi wa Sagalla wanaishi kwa hofu.

“Hatuwezi kuendelea na maisha yetu ya kila siku: kuchota maji, kutafuta kuni wala kwenda shambani!” akasema.

Aliwalaumu maafisa wa Shirika la Wanyamapori (KWS) kwa kushindwa kuwadhibiti ndovu hao, na badala yake “wanawafukuza hadi viungani mwa kijiji na kuwaacha hapo, kisha ndovu wanarejea tena.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.