Serikali imejiandaa vilivyo kwa mtaala mpya- Katibu

Wizara yatoa hakikisho kwamba mfumo mpya wa elimu utatekelezwa kirasmi kuanzia Januari

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA OUMA WANZALA

SERIKALI imejitokeza na kuwahakikishia Wakenya kuwa iko tayari kutekeleza mtaala mpya wa elimu mwezi ujao.

Wizara ya Elimu pia ilisema maafisa wake wanashirikiana na wataalamu kutoka nje katika mchakato wa kufanikisha utekelezaji wa mtaala huo utakaotumiwa kutekeleza mfumo mpya wa elimu.

Katibu wa Wizara hiyo Belio Kipsang’ ambaye alikuwa akiongea Alhamisi usiku alisema serikali imekuwa ikijiandaa kwa uzinduzi wa mtaala huo kwa miaka mingi.

“Tumetekeleza mpango wa kuwaandaa walimu pamoja na kushauriana na wazazi na wadau wengine. Tumefanya yale yote tuliyopaswa kufanya,” akasema Dkt Kipsang alipohutibu katika Mdahalo kuhusu Uongozi ulioandaliwa na Shirika la Habari la Nation (NMG) katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Hata hivyo, wadau wameibua malalamishi kuhusu kiwango cha maandalizi ya walimu, wanafunzi na wazazi kuelekea utekelezaji wa mfumo huo mpya utakaoanza katika Gredi ya 1 hadi Gredi ya 3.

Lakini Dkt Kipsang alisema serikali imetekeleza wajibu wake na iko tayari kwa utekelezaji wa mtaala huo ambao unaegemea zaidi katika kunoa talanta za wanafunzi.

“Mafunzo na uhamasisho wa walimu haukua tukio la siku moja, ni mchakato wa uliochukua muda mrefu. Tumekuwa tukiwafundisha walimu kuwaandaa kwa uzinduzi rasmi wa mtaala mpya,” akaongeza katibu huyo wa wizara.

Dkt Kipsang’ alisema serikali itaendelea kuelekeza rasilimali zaidi katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora.

Aliongeza kuwa serikali pia itaendelea kuongeza bajeti ya elimu kwa sababu ya wajibu wake mkubwa katika kufanikisha maendeleo nchini.

Katibu huyo wa Wizara ya Elimu alifichua kuwa katika mwaka ujao wa kifedha, serikali itatenga Sh468 bilioni kwa sekta ya elimu ikilinganishwa na Sh442 zilizotengwa kwa mwaka huu.

Wengine walioshiriki mdahalo huo ni Afisa Mkuu Mtendaji wa NMG Stephen Gitagama na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuandaa Mtaala Nchi (KICD) Julius Jwan.

Wengine walikuwa mtaalamu wa elimu ya walio na mahitaji maalum Eva Naputuni Nyoike, Msaidizi wa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi Prof Julius Ogeng’o.

Dkt Kipsang’ alikiri kuwa sio shule zote nchini zina miundo msingi bora lakini akasema serikali inafanya kila iwezalo kuimarisha hali hiyo.

Picha/ Sila Kiplagat

Katibu katika wizara ya Elimu Belio Kipsang akihutubu katika kongamano kuhusu Uongozi lililoandaliwa na Shirika la Habari ya Nation katika Chuo Kikuu cha Nairobi Alhamisi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.