Serikali yashauriwa ilinde maslahi ya wanablogu

Taifa Leo - - Habari Za Kaunti - NA THOMAS RAJULA

SERIKALI imeshauriwa kutumia ushawishi mkubwa wa mitandao ya kijamii humu nchini kuwapa motisha vijana na kudhibiti sekta hiyo.

Mtaalamu wa elimu na mwasisi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya Prof Simon Gicharu, aliirai Wizara ya Vijana kutumia maarifa ya wanablogu kwa kuanzisha taasisi ya uanablogu kudhibiti na kuwaelimisha vijana.

Mtindo wa uanablogu, ambao awali ulitengewa tovuti mahususi, sasa umemezwa na mitandao ya kijamii ambapo umejizolea wafuasi wengi.

Akihutubu katika sherehe ya 15 ya mahafali ya chuo hicho, Prof Gicharu alisimulia masikitiko yake baada ya kushuhudia wanablogu wakiteswa na kutumiwa kama matambara mabovu, hasa na wanasiasa na wafanyabiashara maarufu.

“Wanapokamilisha kazi waliyopewa, ya muda tu mfupi, wao huachwa bila malipo. Baada ya hili, wao hukasirishwa na mwenendo huo na nimewashuhudia wakilipiza kisasi dhidi ya watu hao waliowatumia na kuwasahau. Wengine wamekuwa wakikamatwa,” akasema mtaalamu huyo.

Mwanablogu maarufu Cyprian Nyakundi ni mmoja wa wale waliokumbana na mkono wa sheria mara kadha, na hadi sasa ana kesi mahakamani.

Prof Gicharu alieleza kuwa, kutokana na ongezeko la mauzo ya kidijitali mitandaoni, itakuwa wazo zuri iwapo serikali itatenga fedha katika mwaka wa kifedha ujao kuunda taasisi ya kudhibiti na kulinda masilahi ya wanablogu humu nchini.

Kila sekta ya uchumi huhitaji kudhibitiwa, na tunapozidi kupiga hatua katika enzi hii ya dijitali, wadau wa uanablogu wanastahili kulindwa kisheria.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.