Mzee Kirungu amemmiminia Man Giddy baraka gani zinazonata hivi?

Taifa Leo - - Kinaya - Douglas Mutua [email protected]

KWENU kijijini kuna msichana fulani aliyechezeshwa ngoma na karibu kila mtu miaka iliyopita ila sasa hata salamu za Mungu hapati?

Je, yupo mwanamke aina ya ‘zilizopendwa’ ambaye sasa haambiwi “jambo” na yeyote kwa maana watu wamemchoka wakatafuta wengine warembo kumzidi?

Yupo aliyewatishia kwa urembo na kupendeka siku hizo na sasa amechakaa kama matatu ya miaka ya ’90?

Umewahi kujiuliza hali yake ya sasa imetokana na nini, akajipata kwenye mataa baada ya wanaume kuingia mitini?

Imekuwaje hakupata wa kumuoa ilhali waliomtamani ni wengi? Labda alisifiwa urembo akadhani utadumu milele, akaringia kila mtu, hatimaye akaachwa na kila mtu?

Naamini kila kijiji kina mwanamke wa aina hiyo. Hata chetu, lakini sitaji majijna hapa kwa sababu tatu: Sitaki kumpa umaarufu, sitaki kushtakiwa na sina haja kumtambulisha mshamba kwako!

Hata hivyo, kwa sababu naamini wewe u mdau katika siasa za nchi hii, hapa nitamtaja mtu aliye katika hatari ya kujipata kwenye mataa kama mrembo wa miaka hiyo.

Ukikutana na Man Giddy huko vichakani akiwinda ndege kwa bunduki, mwambie mwandishi wa Kinaya amemtahadharisha: Kutongozwa si kupendwa! Juzi alitongozwa na Babu RAO, jana na MADVD, leo na Wiper. Hata Sultani Mwitu amejaribisha.

Wote wanasemekana wataunda ushirika wa kisiasa naye, ama awasaidie au asaidiwe kuingia Ikulu!

Hebu tuulizane: Kwani Man Giddy ana uwezo gani kisiasa? Amekuwaje wa kumtamanisha kila mtu ghafla, wote wakawa wanapigania kunasibishwa naye?

Ni baraka gani hizi kutoka kwa Mzee Kirungu wanazotafuta watongozaji hao ambazo hazikuifaa Kenya kwa miaka 24, eti sasa wazipate kupitia Man Giddy?

Sikiliza na usikilize kwa makini: Hii ni ile pupa ya wacheza densi wa kijijini kumng’ang’ania mrembo mmoja wakasahau wapo wengine gizani wasiopendeza sana, lakini ngoma yao ni ileile au bora zaidi!

Siku hizo za ujana wetu, alipotokea msichana mmoja pekee mrembo zaidi kwenye densi, vidume wa kijijini walimwagika hapo kama maji ya mvua!

Nakwambia waligongana vichwa, aliye na bahati akachomoka naye msijue kilichoendelea huko hadi densi nyingine itakapoandaliwa na sinema ya mwanzo ijirudie.

Huku hayo yote yakiendelea, wasichana wasiong’ang’aniwa walipata wa kuwapenda kimyakimya, sikwambii leo wana waume na watoto na wanaishi kwa raha.

Kumbuka nimekwambia yule wa kung’ang’aniwa angali peke yake, amechakaa na hana wa kumng’ang’ania tena!

Tuelezane ukweli: Hizi juhudi nyingi za kumsawiri Man Giddy kama mwokozi wa nchi hii ni njama za kipumbavu tu za kumkosesha Kipchirchir Samoei malazi ya Ikulu hapo 2022.

Man Giddy anatafutwa na waliowahi kuvaa nembo ya Kanu kwa hisani ya baba yake, wanaomini ile miujiza ya Mzee Kirungu kushinda chaguzi amerithi mwanawe.

Nitacheka mpaka mbavu ziniteguke pale Samoei atakapoingia Ikulu kimyakimya, ghafla usikie waliomtongoza Man Giddy wamesalimiana na Samoei usiku!

Hapo ndipo Man Giddy atabaki kwenye mataa, aitwe zilizopendwa, apokonywe uongozi wa Kanu, watu waache kwenda kumkongoja babake, aisahau Ikulu kama alivyolisahau titi la mama!

Ukimwona mwambie ajue siasa huhitaji uzoefu, si jina kubwa pekee.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.