Mapendekezo ya ODM kuhusiana na mageuzi ya kikatiba kuibua joto kwa wafuasi wa Ruto

Taifa Leo - - Jamvi - NA BENSON MATHEKA

MAPENDEKEZO ya chama cha ODM kwa Kamati ya Uwiano wa Kitaifa (BBI) ambayo kinataka rais awe akiteuliwa na wabunge miongoni mwa mengine, yanatarajiwa kuzua mdahalo mkali ikizingatiwa kwamba kambi ya Naibu Rais William Ruto imekuwa ikipinga marekenbisho ya kikatiba.

Japo kamati kuu ya ODM (NEC) imesema kwamba mapendekezo hayo yangali yanatathminiwa kabla ya kuwasilishwa kwa kamati hiyo iliyoundwa baada ya muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga, itabidi kura ya maamuzi ifanywe ili kutekeleza yakikubaliwa.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho tayari wamefika mbele ya kamati hiyo na kuunga msimamo wa Bw Odinga.

Wadadisi wa kisiasa wanasema japo mapendekezo hayo hayajawasilishwa rasmi mbele ya kamati hiyo inayoendelea kukusanya maoni kutoka kwa umma kwa wakati huu, ni wazi kuna tofauti kati ya kambi ya Bw Ruto na Bw Odinga.

“Hilo limekuwa wazi. Kwamba kuna tofauti kati ya Bw Odinga na Bw Ruto hasa kuhusu kura ya maamuzi. Wawili hao na washirika wao wamekuwa wakizozana hadharani kuhusu pendekezo hilo na malumbano kati yao yanatarajiwa kupamba moto ripoti ya kamati itakapoandaliwa,” asema wakili Charles Atiko mdadisi wa masuala ya siasa.

Anasema kulingana na ripoti za vyombo vya habari kwamba ODM inapendekeza Rais kuchaguliwa na bunge na kuhudumu kwa kipindi kimoja pekee cha miaka saba, katiba lazima ibadilishwe.

“Hauwezi kutarajia kambi ya Bw Ruto kuchukulia pendekezo kama hili kwa urahisi ikizingatiwa kuwa anatarajia kumrithi Rais Kenyatta ambaye atakamilisha vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja 2022. Bila shaka madahalo kuhusu pendekezo kama hilo utaibua joto kali la kisiasa,” alisema Bw Atiko.

Kulingana na rasimu ya mapendekezo ambayo chama hicho kimeandaa, bunge linapaswa kuwa na wabunge 180 huku seneti ikiwa na wanachama 29 pekee. Hii inamaanisha kuwa nafasi zilizotengewa wanawake na makundi ya vijana na walemavu vitaondolewa jambo ambalo litazua hisia kali kutoka kwa mashirika ya kutetea haki.

Kwa sasa kuna wabunge 419 wakiwemo maseneta. Wadadisi wanasema pendekezo la chama cha Raila kwamba kuwe na viwango vitatu vya utawala litapandisha joto la kisiasa ikitiliwa maanani kwamba Bw Ruto na magavana wamekuwa wakilipinga vikali waziri huyo mkuu wa zamani alipolipendekeza kwenye kongamano la ugatuzi Kaunti ya Kakamega mapema mwaka huu.

Kulingana na Bw Odinga, nchi inapaswa kugawanywa kwa majimbo 14 yanayohusisha kaunti kadhaa, yanayosimamiwa na waziri mkuu wa majimbo na naibu wake watakaochaguliwa na mabunge ya kaunti zitakazounda kila eneo.

Tayari magavana wawili wa ODM eneo la Pwani, Amason Kingi wa Kilifi na Hassan Joho wa Mombasa, tayari wameunga utawala wa majimbo japo chama bado hakijawasilisha mapendekezo yake mbele ya kamati kikisema kinahitaji kuyachanganua zaidi.

Baadhi ya magavana wanahisi kuwa kubuniwa kwa kiwango cha tatu cha utawala, kutapunguza mamlaka yao na kuongeza gharama.

“Kuwa na viwango vitatu vya utawala ni kuongeza mzigo kwa mlipa ushuru. Ninaamini ugatuzi ulivyo, unafaa kuimarishwa kwa kutengewa pesa zaidi za maendeleo badala ya kubuni kiwango kingine kwa lengo la kupunguza mamlaka ya magavana,” aeleza gavana mmoja kutoka Rift Valley ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Alipohutubia kongamano la ugatuzi mnamo Aprili mwaka huu, Bw Ruto alikataa pendekezo hilo akisema ni sawa na kupanga upya mfumo wa utawala wa ugatuzi.

“Ugatuzi ni kupeleka utawala na rasilmali mashinani zaidi na hatuhitaji kubadilisha katiba ili kufanya hivyo,” alisema Bw Ruto.

Kulingana na wadadisi, mapendekezo yoyote yatakayotumiwa na kamati ya uwiano kuandaa ripoti yake, lazima yatazua mdahalo. Chama cha ODM pia kinataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ifanyiwe marekesbisho na kuwe na mfumo wa kuajiri na kuteua wafanyakazi wa umma utakaohakikisha usawa wa kikabila na kimaeneo. Kinasema kwamba mfumo wa serikali wa ubunge utamaliza uhasama wa kikabila na ghasia ambazo huwa zinazuka kila wakati wa uchaguzi.

Katibu mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna mnamo Jumanne alisema mapendekezo hayo yananuiwa kuzua mjadala kabla ya kuidhinishwa na kuwasilishwa kwa kamati ya uwiano. Hata hivyo, viongozi wa chama hicho wanaofika kutoa maoni yao binafsi mbele ya kamati hiyo wamekuwa wakitoa mapendekezo sawa ishara kwamba wanaunga msimamo wa chama. Kinara wa Nasa Raila Odinga katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna seneta wa Siaya James Orengo na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen wakiwa kwa mazishi Willy Kaino Kilimo, babake Mwekahazina wa ODM Ogla Karani eneo la Chebai, Elgeyo-marakwet miezi tisa iliyopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.