Masaibu ya babu Nyakebagendi mikononi mwa polisi wa trafiki (Sehemu ya 2)

Taifa Leo - - Jamvi - NA NYARIKI ENOCK NYARIKI

KIMYA kingi. Kimya ambacho kingemfanya yeyote aliyekuwa basini kukisikia kishindo cha pamba iliyoanguka kwenye sakafu ya basi. Babu Nyakebagendi alikuwa amezisikia habari za sheria za usafiri kwenye redio yake kweche ya sanyo ingawa hakika hakujua kwamba vyombo vya serikali vilikuwa mbioni kuzitekeleza. Sasa asingeweza kukifunua kinywa chake kumwambia yule afisa wa polisi kwamba alikuwa ameivunja sheria. Si huko kutakuwa kujinasa kwa ulimi wake mwenyewe? Alikaa tutwe, yeye na abiria wenzake.

“Sajenti Gunge!’’ Inspekta aliamuru na kukivunja kimya kile.

“Afande!” Sajenti Gunge aliitika kwa kusimama wima na kupiga saluti.

“Lisindikize basi hili hadi kituoni. Chawa katika seli yetu ya polisi watapata kazi ya kufanya usiku kucha!’’

Maneno yale yaliifanya michango ya Babu Nyakebagendi kujawa na upepo uliopita kwa kasi na kulifanya tumbo kutoa sauti iliyofanana na mngurumo wa mvua. Masimulizi aliyokuwa ameyasikia kutoka kwa marafiki zake kuhusu masaibu yaliyokuwa yamewakumba kwenye seli na korokoro za polisi siku hiyo yalimfika yeye. Alijihesabu miongoni mwa watu walioamkia mkono mbaya wa kitanda Ijumaa ile.

Hata hivyo, babu alikuwa na kila sababu ya kutabasamu. Punde tu basi lilipoegeshwa nje ya uwanja wa kituo cha polisi, afisa aliyekuwa zamuni alifanya hima kuyaandikisha majina ya abiria kwenye kitabu cha OB. Kisha, wote walitiwa kwenye karandinga la polisi na kusafirishwa hadi kwenye mahakama ya Vilimani.

Hakimu aliyeisikiliza kesi ya ‘washukiwa’ alikuwa na wakati mgumu wa kuwatuliza watu walioangua vicheko mahakamani kutokana na majibu ya wale abiria dhidi ya kesi iliyowakabili. Wapo waliosema kwamba hawakuwa na habari kuhusu zile sheria mpya. Baadhi yao walisema kwamba hawakujua kuwa ni hatia kutofunga mkanda wa usalama. Jibu la Babu Nyakebagendi ndilo lililoifanya korti kulipuka kwa kicheko cha radi.

“Mzee, kwa nini hukufunga mkanda wa usalama?’’ hakimu alimwuliza.

Babu Nyakebagendi alikishtua kichwa chake kuelekeza upande wa kulia na kukiegemeza kwenye bega lake. Kisha alijibu, “Mheshimiwa hakimu, basi lilipoanza safari kutoka Nungunungu, hatukuwaona maafisa wowote kwenye vizuizi vya polisi hadi pale lilipokuwa linaingia mjini Buzungu.”

“Mzee, ina maana kuwa wewe hufunga mkanda wa usalama kwa sababu ya kuwaogopa polisi?’’ hakimu alimwuliza.

Washtakiwa walitozwa faini ya shilingi elfu tano, elfu tano kila mmoja, kwa hatia ya kuvunja sheria mojawapo ya trafiki. Shilingi elfu tano ndizo pesa za pekee alizokuwa nazo Babu Nyakebagendi. Tena, hazikuwa pesa zake bali zile alizopewa na Bibi Hannah ili akamnunulie bidhaa kwa ajili ya sikukuu ya kuzaliwa kwake. Alipokuwa akiondoka mahakamani, Babu Nyakebagendi alizama kwenye biwi la mawazo. Angemwambia nini mkewe kuhusu bidhaa alizokuwa ametumwa?

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.