18 wauawa na wafuasi wa kundi la wapiganaji la ADF

BENI, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

Taifa Leo - - Habari Za Afrika Na Dunia - Na MASHIRIKA

WATU 18 waliuawa na wafuasi wa kundi moja la wapiganaji mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), msemaji mmoja wa jeshi la nchi hiyo alisema.

Shambulio hilo lilitekelezwa Ijumaa jioni katika eneo hilo ambalo limeathirika zaidi na maradhi hatari ya Ebola.

Watu 12 walifariki katika kitongoji cha Mangolikene viungano mwa mji wa Beni, Kivu Kaskazini huku wengine sita wakiuawa majira ya usiku katika eneo la Paida, meya Nyonyi Masumbuko Bwanakana aliwaambia wanahabari.

Msemaji wa jeshi katika eneo hilo Mak Hazukay alisema wanashuku mauaji hayo yalitekelezwa na wapiganaji wa kundi la waasi la ADF.

“Mauaji ya watu watano katika eneo la Paida yalitokea wakati ambapo wafuasi wa kundi hili walijaribu kuvamia kambi ya kijeshi. Tumeanzisha operesheni kali ya kuwasaka wapiganaji hao,” Kapteni Hazukay alisema.

Na mwakilishi wa kundi moja la kutetea haki za umma katika eneo la Paida alisema milipuko ilisikika eneo la Paida usiku wa kuamkia Ijumaa, saa chache kabla ya mauaji hayo kutekelezwa.

Serikali imekuwa ikilaumu kundi hilo kwa visa vya mauaji, wizi wa kimabavu na utekaji nyara katika jimbo hilo la Kivu Kaskazini. Hata hivyo, nyakati fulani, washambuliaji halisi huwa hawajulikani.

Kundi la ADF (Allied Demokratic Forces) ni kundi la kiislamu lenye asili yake nchini Uganda ambalo uongozi wake haujulikani japo limewaua mamia ya watu DRC tangu mwaka wa 2014.

Lakini wachanganuzi wanasema wafusi wa ADF hutekeleza mashambulio katika eneo hilo kwa malengo mbalimbali. Mashambulio hayo yamelemaza juhudu za serikali za kupambana na kuenea kwa maradhi ya Ebola.

Kufikia sasa inaaminika kuwa watu 471 wameambukizwa huku 273 wakifariki kutokana

na ugonjwa huo hatari.

Wizara ya Afya ya DRC ilitangaza watu wengine 13 waliambukizwa maradhi hayo Ijumaa pekee. Hii ni idadi kubwa zaidi ya

watu kuambukizwa kwa siku moja tangu mkurupuko wa ugonjwa huo kutangazwa rasmi mnamo Agosti mwaka huu

Mashambulio ya Ijumaa yalijiri siku moja baada ya mgombeaji urais wa upinzani Martin Fayulu kuzuru mji wa Beni kuzindua kampeni yake kuelekea uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Bw Fayulu ni miongoni mwa wagombeaji 21 wanaowania nafasi ya kutwaa kiti cha urais kuchukua nafasi ya Joseph Kabila ambaye ameongoza taifa hilo tangu mwaka wa 2001.

“Mauaji ya watu watano katika eneo la Paida yalitokea wakati ambapo wafuasi wa kundi hili walijaribu kuvamia kambi ya kijeshi.” Msemaji wa Jeshi Mak Hazukay

Picha/ AFP

Wafuasi wa Kiongozi wa Upinzani nchini DR Congo Martin Fayulu waonyesha furaha kukutana naye wakati wa kampeni za urais je ya jiji la Kinshasa wiki iliyopita. Mashambulio ya Ijumaa yanajiri siku moja baada ya Fayulu kuzuru mji wa Beni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.