Ndoa ni safari

Taifa Leo - - Ushairi Wenu -

Ndoa kweli ni safari, tuombeane na dua, Atuepushe na shari, tusije pigwa na jua, Isitufike hatari, bila ya sisi kujua,

Ndoa kweli ni safiri, isohitaji nauli.

Inaponyesha mvua, hata na jua kutua, Visa tusije ibua, yasiyofaa kuyazua, Nikukinge nalo jua, nisitiri kwa mvua, Ndoa kweli ni safari, isohitaji nauli.

Chumbani nikirejea, kwangu wewe sogelea, Viatu ukinivua, mzigo nikiutua,

Kwako kinda nimetua, hata nawe unajua, Ndoa ni kama safari, isohitaji nauli.

Yahitaji vumilivu, ni sugu ino safari, Penzi ongezea wivu, kila siku ikijiri, Subiri tuile mbivu, usitoe yangu siri, Ndoa kweli ni safari, isohitaji nauli.

Hivi leo tukipata, tushukurie Jalia, Akitujalia bata, tule tukifurahia, Tukikosa mlo hata, nakuomba vumilia, Ndoa kweli ni safari, isohitaji nauli AYIEKO JAKOYO ‘Malenga wa Bara’ Mumias Mjini

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.