Ukiteuliwa waziri

Taifa Leo - - Ushairi Wenu -

Jamani wanasiasa, muweze kuwa wazuri, Kazi mkipewa sasa, sianze chenu kiburi, Kutulaghai we asa, wangu uno ushauri, Kiteuliwa waziri, tekeleza wajibuwo.

Situleteye uchama, maana hatutaula, Jitahidi fanye wema, kufaidi makabwela, Uwe mwingi wa huruma, takubarikia Mola, Kiteuliwa waziri, tekeleza wajibuwo.

Nchini weye zunguka, usibaki pale pale, Mengi utayakumbuka, tamati tapokikile, Mapema sana rauka, tangulia uwe mbele, Kiteuliwa waziri, tekeleza wajibuwo.

Sikuzuie yeyote, miradi kuendeleza,

Hujazuiwa popote, katiba vyema yeleza,

Uhuru unao wote, yangu hayo memaliza, Kiteuliwa waziri, tekeleza wajibuwo.

MUKOYA AYWAH ‘Malenga Mpelelezi’ Kigango, Thika

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.