Juventus wakamata kilele kwa kani

Taifa Leo - - Spoti - TURIN, ITALIA

BAO la mvamizi Mario Mandzukic liliwapa Juventus ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Inter Milan katika mchuano wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Ijumaa.

Ushindi wa Juventus ambao wanawinda ubingwa wa Ligi Kuu ya msimu wa nane mfululizo, uliwawezesha kufungua pengo la alama 11 kileleni mwa jedwali.

Mandzukic alikamilisha kwa ustadi krosi ya Joao Cancelo katika kipindi cha pili baada ya Inter kupoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo, zingewavunia alama tatu muhimu mwishoni mwa mchuano huo.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa, nyota Mauro Icardi (kushoto) wa Inter Milan aruka juu ya Mario Mandzukic wa Juventus kwenye mechi ya Serie A ugani Stadio delle Alpi, Ijumaa. Roberto Gagliardini alishuhudia kombora lake likibusu mwamba wa lango la Juventus huku Matteo Politano akishindwa pia kuchuma nafuu kutokana na masihara ya kiungo Blaise Matuidi.

Kufikia sasa, Juventus wanashikilia kwa pamoja na PSG rekodi ya kutoshindwa katika mechi 15 za ufunguzi wa kampeni za msimu, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na kikosi chochote kingine katika historia ya Ligi Kuu tano za bara Ulaya.

Matokeo ya Ijumaa yaliwasaza Inter katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 14 nyuma ya viongozi Juventus ambao pia hawajapoteza mchuano wowote wa nyumbani tangu Aprili 2018.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.