Kibwana, Ngilu na Mutua wapanga njama ya kumng’oa Kalonzo

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na KITAVI MUTUA

MAGAVANA watatu kutoka eneo la Ukambani wanapanga kuandaa mikutano ya hadhara katika kaunti zao, ili kueleza wafuasi sababu yao kutaka ‘kumtaliki’ kisiasa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kuchukua mkondo mwingine wa kisiasa.

Watatu hao, Dkt Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Prof Kivutha Kibwana (Makueni) wamepanga kuandaa msururu wa mikutano hiyo, kwa kongamano moja kubwa ambalo litahusisha wanachama wa mabunge ya kaunti hizo tatu, ili kujadili masuala ya kiuchumi ya eneo hilo.

Mikutano ya hadhara ya pamoja ya viongozi hao, kupitia kwa muungano wa eneo hilo wa kiuchumi wa SEKEC itatoa fursa kwao kujadili masuala ya kijamii na kiuchumi ambayo yamekuwa yakiathiri eneo hilo, huku pia wakitarajiwa kuzungumzia suala la ‘kumtaliki’ kiongozi mkuu wa eneo hilo, Bw Musyoka.

Magavana hao wanatarajiwa kuandaa angalau mkutano mmoja wa hadhara kila mwezi, katika hatua inayoonekana kama kuanza kuzua pingamizi kuhusu umiliki wa chama cha Bw Musyoka eneo hilo.

“Tutazunguka tukiwaambia watu kile kizuri kwao kisiasa na kuhusu maendeleo kwani sisi ndio viongozi tuliochaguliwa wa jamii hii na tuna idhini ya umma ya kuongoza bila kutafuta ruhusa ya yeyote,” akasema Dkt Mutua. Awali wiki hii, viongozi hao walikutana eneo la Kivandini, Machakos, ambapo walieleza kuwa jamii ya Wakamba inahitaji uongozi mpya, ambao unalenga kuitafutia maendeleo na kutetea rasilimali za kitaifa kupelekwa huko.

Leo, watatu hao, aidha wanatarajiwa kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa Katoliki la Katutu, eneo la Kitui Magharibi, kisha wahutubie umma katika soko la Kabati.

“Kwa Wakamba na Wakenya kwa jumla kuhisi matunda halisi ya uhuru, sharti tubadili aina ya viongozi tunaowachagua kutuongoza na kuzungumza kwa niaba yetu,” akasema Dkt Mutua. Prof Kibwana alipuuzilia matamshi ya baadhi ya viongozi wa eneo hilo kuwa kiongozi mwingine kutoka eneo hilo kulenga kutafuta urais ni usaliti kwa jamii ama kumharibia Bw Musyoka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.