Maswali Omamo akisoma hotuba ya Rais mbele ya Ruto

Taifa Leo - - FRONT PAGE - JUSTUS OCHIENG na BENSON MATHEKA

Ukiukaji wa itifaki ulishuhudiwa jana wakati Waziri wa Ulinzi Rychelle Omamo aliposoma hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta mbele ya Naibu Rais William Ruto.

Katika tukio lililoshangaza wengi kwenye sherehe ya kutawazwa kwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kisumu Philip Anyolo, Bw Ruto alihutubu kisha akamwalika Bi Omamo kusoma hotuba ya Rais.

Ilitarajiwa kuwa akiwa Naibu Rais, Bw Ruto angeongoza maafisa wengine wa serikali kumwakilisha Rais na kusoma hotuba yake sawa na inavyofanyika katika hafla za awali.

Hata hivyo, alipoalikwa na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, Bw Ruto alizungumza kisha akamwalika Bi Omamo kusoma hotuba ya Rais. Hii ilichukuliwa na wengi kwamba ni Waziri Omamo aliyetumwa na Rais kumwakilisha katika hafla hiyo.

Baadhi ya Wakenya walitaja tukio hilo kama ukiukaji mkubwa wa itifaki.

“Ni masuala ya kufurahisha haya... Mheshimiwa Raila anamwalika Naibu Rais kuzungumza, Naibu Rais anazungumza na kumwalika Waziri Rachael Omamo kuwasilisha hotuba ya Rais... ningeapa kuwa kazi ya naibu ni unaibu,” mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo ambaye alihudhuria hafla hiyo aliandika kwenye Twitter.

Ni mara ya kwanza tangu 2013 Jubilee ilipoingia mamlakani tukio kama hilo kushuhudiwa huku baadhi ya Wakenya wakisema linadhihirisha kuwa uhusiano wa Rais Kenyatta na Bw Ruto umekuwa baridi.

Wawili hao hawajaonekana hadharani pamoja mwaka huu. Chama chao cha Jubilee pia kimekumbwa na mzozo baadhi ya viongozi na wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya wakiapa kumzuia Ruto kugombea urais.

Hii imezua mgawanyiko katika chama hicho tawala. Katika hotuba yake Rais Kenyatta aliwataka viongozi wa kidini kusaidia kuunganisha Wakenya.

“Ninaomba kanisa kuendelea kupiga ufisadi vita na maovu mengine kwa nguvu zaidi,” alisema Rais Kenyatta.

Wakati huo huo, Dkt Ruto alimpa zawadi ya Mitsubishi Pajero Askofu Philip Anyolo baada ya kusimikwa kama Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kisumu.

Naibu Rais alisema gari hilo litamsaidia kuzuru maeneo tofauti eneo hilo.

“Kama kiongozi wa dini atakayeenda maeneo ya mbali kaskazini mwa Kenya kutoka Turkana, Kisumu hadi Migori, tumeamua kuja pamoja na kukupa gari la kukusaidia kutembelea watu eneo lako,” alisema.

Bw Ruto alisema ununuzi wa zawadi hiyo ulitokana na mchango wa Rais Uhuru Kenyatta, viongozi kutoka eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa na wengine kutoka Magharibi.

Naibu Rais William Ruto asemezana na kinara wa ODM Raila Odinga kwenye ha a ya kumtawaza Askofu Mkuu wa Jimbo la Kisumu Philip Anyolo katika Chuo Kikuu cha Uzima, Kisumu jana. Picha/ondari Ogega

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.