Hakuna mkataba wa Uhuru kuunga Ruto 2022-Duale

Asema wawaniaji wote watajitosa uwanjani kuwania tiketi

Taifa Leo - - FRONT PAGE - NA KIPCHUMBA SOME

BAADA ya kimya cha muda mrefu licha ya misukosuko katika chama cha Jubilee, mbunge wa Garissa mjini na kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale amezungumza, japo maneno yake yakiibua shaka kuhusu mustakabali wa chama hicho.

Kwa mara ya kwanza, Bw Duale amekiri kuwa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto hawakuandikiana mkataba wowote kuwa Bw Ruto atapokea mamlaka ya chama kuwania Urais moja kwa moja, akisema yeyote atakayetaka tiketi ya kuwania Urais atajitosa katika debe la uchaguzi wa chama.

Kiongozi huyo, ambaye ni mwandani mkubwa wa Bw Ruto, kwa tahadhari kubwa aidha alisema kuwa naibu wa Rais atategemea rekodi ya maendeleo ya serikali ya Jubilee kuanzia 2013 kujipigia debe itakapofika 2022, badala ya kudai ‘deni la kisiasa’ kutoka ngome ya Rais Kenyatta.

“Ninavyojua ni kuwa hakukuwa na Mkataba wowote wa Maelewano (MOU) ulioandikwa kati yao (Rais na naibu wake) kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022. Aidha, hakuna deni lolote la kisiasa ambalo yeyote anadai mwingine,” akasema Bw Duale.

Alisema kuwa Rais Kenyatta na Bw Ruto waliwania uongozi wa nchi kwa pamoja mnamo 2013 na 2017 kutokana na maelewano ya kimaono baina yao, wala haikuwa kutokana na mkataba wowote.

Bw Duale hakueleza moja kwa moja ikiwa, kulingana naye, Rais Kenyatta atamuunga mkono naibu wake kutafuta Urais moja kwa moja, akisema kuwa sheria ya chama ndiyo itazingatiwa kutafuta mwaniaji wa Jubilee.

“Muundo wa chama na katiba viko wazi kabisa kuhusu chaguzi zote 22. Kutoka mwaniaji wa Urais hadi wa uwakilishi wadi wote watapitia uchaguzi wa mchujo huru, haki na wenye uwazi. Hiyo ndiyo ilikuwa hali kwenye uchaguzi wa 2017. Hivyo basi, naibu Rais sharti ajiandae kupambana na yeyote ambaye atajitokeza kutafuta tiketi ya Urais kupitia sheria za chama,” akasema.

Licha ya tofauti zinazoshuhudiwa katika chama hicho na ambazo zimetawala nchi katika siku za karibuni, kiongozi huyu alishikilia kuwa uhusiano baina ya Rais na naibu wake bado hauna dosari.

“Kama mwandani wao wote, nawahakikishia kuwa kila kitu kiko sawa katika chama chetu. Kile tunachoshuhudia ni sauti tofauti za kisiasa ambapo ni kawaida katika siasa za Kenya. Hakuna sababu ya kuwa na shaka,” Bw Duale akasema.

Lakini licha ya hakikisho lake, kiongozi huyu alisema kuwa viongozi ambao wamekuwa wakitoa matamshi yanayokiuka katiba ya chama wataadhibiwa. Wabunge Moses Kuria wa Gatundu Kusini na Kimani Ngunjiri wa Bahati wakiorodheshwa kuwa waliopotoka.

“Jubilee ni chama cha kitaifa na tunaruhusu uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kwa wanachama wetu. Lakini matamshi ya kiholela yaliyotolewa na Moses Kuria, David Murathe (ambaye alijiuzulu kama naibu mwenyekiti wa Jubilee) na Kimani Ngunjiri ambayo yanavuruga chama hayatakubalika. Tutachukua hatua za adhabu zinazofaa dhidi yao kulingana na katiba,” akasema.

Mbunge huyo alisema kuwa chama hicho hakina mpango wowote wa kuandaa kikao na wanachama wake kwa ajili ya kusuluhisha tofauti ambazo zimeshuhudiwa, akisisitiza kuwa Jubilee bado iko pamoja.

“Lakini kiongozi wa chama akiitisha mkutano wa aina hiyo, uongozi wa juu wa Jubilee uko tayari kuandaa,” akaongeza.

Picha/maktaba

Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale (kushoto) akihutubu hapo awali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.