JUHUDI ZA KUOKOA NDOA YA JUBILEE

Makundi kadhaa yapanga kukutana na Rais na Ruto yakisema zogo laweza kukwamisha shuguli za serikali

Taifa Leo - - FRONT PAGE - Na JUSTUS WANGA

Juhudi za kuokoa chama cha Jubilee kisisambaratike zimeanza huku kukiwa na hofu kwamba mzozo unaoendelea katika chama hicho unaweza kulemaza shu-

kulemaza shughuli za serikali.

Makundi matatu yanajitahidi kuwapatanisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ambao, inashukiwa, uhusiano wao umekuwa baridi siku za hivi punde.

Hata hivyo, makundi matatu yaliyojitolea kuwapatanisha, kila moja linasukumwa na ajenda zake.

Kundi la kwanza ni la wanachama wenye msimamo wa kadri, la pili ni la viongozi wa makanisa na wazee, na la tatu linahusisha wafanyabiashara walio na ushawishi.

Huku wazee na viongozi wa makanisa wakidhamiria kuimarisha amani nchini, kundi la wafanyabiashara linahofia kuwa joto la kisiasa litafanya wakose tenda za serikali.

Mnamo Ijumaa, Askofu Maurice Crowley wa Dayosisi ya Kitale ya Kanisa la Katoliki aliongoza viongozi wengine wa makanisa kukutana na Bw Ruto nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu katika juhudi za upatanishi.

“Hali ya baadaye ya nchi inategemea jinsi viongozi wetu wanavyofanya. Tutashirikiana na serikali kuimarisha utawala na kuimarisha maendeleo,” askofu huyo alisema. imegundua kuwa mbali na kuwahusisha viongozi zaidi wa kidini, kundi hilo linafanya juhudi kukutana na Rais Kenyatta kumuomba atulize wandani wake. Pia, wanataka kumweleza hofu ya kambi ya Bw Ruto.

Hata hivyo, mwandani mmoja wa Bw Ruto aliambia gazeti hili kwamba haoni mazungumzo ya upatanishi yakifanyika hivi karibuni.

“Naibu Rais anahisi kwamba ni mapema mno kwa mazungumzo. Anahisi kwamba wale wanaopinga azma yake ya kuwa rais wanafaa kuachwa kupayuka hadi wachoke kabla ya kuketi na kuamua kusuluhisha mambo haya,” alisema.

Kuna wasiwasi kwamba kimya cha Rais kinaweza kuua chama hicho. Huku Rais akishughulika kuacha kumbukumbu nzuri, naibu wake anaweka mikakati ya kushinda urais 2022.

Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki, Simon Mbugua, alimhimiza Rais kuzima mzozo katika chama hicho.

“Haya yote yanatendeka kwa sababu Rais amenyamaza. Anafaa kuzungumza,” alisema.

Nao wanachama wasio na misimamo mikali ya chama wanahisi kwamba vitendo vya kambi zote mbili vitaharibu chama na tayari wamezungumza na Naibu Rais.

Japo hawakutaka tutaje majina yao, walisema wanataka kumtumia mwandani wa Rais Uhuru, Bw Ngengi Muigai kumfikia kiongozi huyo wa nchi.

Mbali na matamshi ya hadharani ya washirika wa Rais, inasemekana Bw Ruto hafurahishwi na jinsi vita dhidi ya ufisadi vinavyoendeshwa. Anaamini kwamba vinalenga washirika wake serikalini.

Jana, waziri mmoja anayesimamia wizara muhimu alisema anahofia uchumi umeanza kudorora kufuatia kupanda kwa joto la kisiasa.

“Hakuna pesa. Uchumi umeanza kuathiriwa na kampeni za mapema,” alisema.

Inasemekana wafanyabiashara wenye ushawishi Jumanne walituma ujumbe kwa Rais wakielezea wasiwasi wao kuhusu taharuki iliyoko na athari zake kwa uchumi.

Wafanyabiashara hao walikuwa wakisubiri kukutana na Rais Kenyatta Nairobi akitoka Mombasa alikokuwa likizoni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.