GOR MAHIA KIFUA MBELE WAKIELEKEA CAMEROON

Taifa Leo - - FRONT PAGE - NA GEOFFREY ANENE

GOR MAHIA ina kibarua kigumu cha kusonga mbele katika soka ya Kombe la Mashirikisho ya Afrika baada ya kukubali New Star ya Cameroon kupata bao la ugenini katika ushindi wao wa 2-1 jijini Nairobi, jana.

Mabingwa hawa wa Kenya mara 17, ambao wana rekodi mbaya dhidi ya klabu za kigeni ugenini ya ushindi mmoja katika mechi 12 zilizopita, waliona lango kupitia Lawrence Juma dakika ya 40. Kiungo huyu wa Gor kisha alisawazisha New Star baada ya kujifunga dakika ya 72 kutokana na kona. Raia wa Rwanda Jacques Tuyisenge alihakikishia vijana wa Hassan Oktay ushindi alipofuma bao la muhimu kichwa kisafi dakika ya 86.

Nao Wakenya Jesse Were na Anthony Akumu walichezea klabu yao ya Zesco United katika ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya miamba wa Afrika Kusini Kaizer Chiefs nchini Zambia, jana. Were alipachika mabao mawili ya mwisho, moja penalti katika kipindi cha kwanza, baada ya Lazarous Kambole kufungua akaunti ya mabao dakika ya 25. Mzimbabwe Khama Billiat alifungia Kaizer bao la kufutia machozi dakika chache kabla ya mapumziko.

Hapo Jumamosi, Mkenya Duncan Otieno alianza mechi ya Nkana FC dhidi ya San Pedro ya Ivory Coast ambayo miamba hao wa Zambia walitawala 3-0 uwanjani Nkana.

Otieno aliajiriwa na Nkana mwisho wa msimu uliopita akitokea AFC Leopards. Mkenya mwingine anayesakatia Nkana, beki Musa Mohamed alikuwa shabiki katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza baada ya kula kadi mbili ya njano nyumbani na ugenini dhidi ya miamba wa Tanzania, Simba SC kwenye Klabu Bingwa Afrika. Nkana ilizamisha San Pedro kupitia mabao ya Ronald Kampamba, Joseph Musonda na Festus Mbewe.

Mohamed, ambaye alipata umaarufu akiwa Gor, atakuwa huru kumenyana na San Pedro katika mechi ya marudiano. Gor, Nkana na Zesco zilijipata katika mashindano haya ya daraja ya pili baada ya kubanduliwa nje ya Klabu Bingwa Afrika mwezi uliopita. Zinatafuta tiketi za kuingia mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho ambalo droo yake itafanywa Januari 21.

Msimu uliopita, Gor ilifika mechi za makundi katika soka hii na kuzawadiwa Sh27.9 milioni baada ya kupigiwa breki katika awamu hiyo. Gor itakuwa makini kulinda nafasi yake katika mashindano haya wakati wa mechi ya marudiano nchini Cameroon isije ikabanduliwa nje na kutoka mikono mitupu. Zawadi za soka hii zinaanzia mechi za makundi hadi fainali.

PICHA/CHRIS OMOLLO

Lawrence Juma wa Gor Mahia ajumuika na Francis Mustafa (kushoto) kusherehekea bao alilowafungia Gor Mahia dhidi ya New Stars De Doula ya Cameroon katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) hapo jana ugani MISC Kasarani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.