Nyong'o apelekwa Nairobi kutibiwa

Taifa Leo - - NEWS - CECIL ODONGO Na CAROLINE MUNDU

GAVANA wa Kisumu, Prof Peter Anyang’ Nyong’o jana alisafirishwa kwa ndege kutoka Kisumu hadi jijini Nairobi kwa matibabu maalum katika hospitali ya Aga Khan. Kulingana na Msimamizi Mkuu wa hospitali ya Aga Khan mjini Kisumu, Dkt Sam Oula, Prof Nyong’o alisafirishwa Nairobi kufanyiwa uchunguzi wa kina wa kimatibabu. “Tulimlaza hapa hospitalini usiku kucha. Ingawa hayuko hatarini kwa sasa, tunahitaji kumfanyia uchunguzi zaidi wa kimatibabu kwa kuwa hatukuwa na matokeo ya mwisho ya uchunguzi wa maradhi yanayomkumba,” akasema Dkt Oyula. Mkuu wa mawasiliano katika ofisi ya gavana, Aloice Ager, awali alisema taarifa kutoka hospitalini ziliwajuza kwamba Prof Nyong’o alikuwa akikumbwa na tatizo kupungua kwa kasi ya mpigo na damu.

Ager alisema gavana aliomba radhi kwenda kutafuta matibabu wakati wa hafla hiyo alipohisi vibaya.

Prof Nypng’o alihisi kizunguzungu wakati wa hafla ya kutawazwa kwa Askofu Philip Anyolo kuwa askofu mkuu wa kanisa katoliki dayosisi ya Kisumu katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Uzima mjini ndipo akakimbizwa hospitalini.

Alilazwa hospitalini humo usiku kucha kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na kutibiwa kabla ya kuhamishwa hadi tawi la hospitali hiyo jijini Nairobi jana asubuhi.

Naibu Rais William Ruto, kinara wa ODM Raila Odinga na baadhi ya mawaziri walihudhuria kutawazwa kwa Askofu Anyolo ambaye awali alihudumu katika dayosisi jirani ya Homabay kabla ya kuteuliwa na Papa Francis kuhudumu Kisumu.

Aliyekuwa askofu wa dayosisi ya Kisumu Zacheaus Okoth, 76, ambaye ni mwanachama wa kamati ya maridhiano maarufu kama 'Building bridges initiative' iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, alistaafu baada ya kuihudumia dayosisi hiyo kwa muda wa miaka 30.

Prof Nyong’o alisafirishwa kutoka hospitalini hadi uwanja wa ndege wa Kisumu kwa ambulensi na kubebwa kwa ndege maalum ya kusafirisha wagonjwa ya AMREF Flying Doctors.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.