Waliopiga kambi katika kituo cha afya walalamikia maisha duni

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na FLORAH KOECH

WATU zaidi ya 200 wanahofia usalama na mkurupuko wa maradhi kutokana na mazingira duni wanayoishi baada ya kurejeshwa katika eneo la Mukutani, Baringo Kusini miezi mitatu iliyopita.

Wakazi hao ambao walikuwa wamehama kufuatia mashambulizi ya wizi wa mifugo, sasa wamelazimika kutafuta hifadhi katika kituo cha afya kilichoachwa cha Mukutani.

Watu hao walikuwa wamepiga kambi katika eneo la Eldume tangu Machi 2017 kufuatia mapigano ya kikabila yaliyosababisha vifo vya watu 11, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Taifa Leo ilipozuru eneo hilo, ilibaini kwamba mamia ya wanawake wakongwe ambao walihamishiwa katika eneo hilo Novemba mwaka jana wanaishi katika hali ya kusikitisha.

Wengi wao walijipata katika hali hiyo baada ya makazi yao kuvamiwa na kuharibiwa na wahalifu kutoka jamii jirani.

Bi Christine Kateiya, alisema baadhi ya familia zilihamia kwa kituo hicho baada ya kupata makazi yao yaliharibiwa na mali yao kuibwa.

Wakazi wachache ambao walipata nyumba zao zikiwa hazijaharibiwa walijitolea kuwasaidia wenzao.

“Tulikuwa tukiishi katika kambi ya muda Eldume, ambayo imo umbali wa zaidi ya kilomita 70 kutoka Mukutani. Tulikuwa tukitoroka mapigano ambapo watu kadhaa waliuawa. Hata hivyo, tulipata nyumba zetu zikiwa zimeharibiwa kabisa na wahalifu tuliporejea,” akasema.

Akaongeza: “Hatukuwa na lingine, ila kupiga kambi katika kituo hiki cha afya, kwani hakikuwa kikitumika kutoa huduma za afya.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.