Vikundi 2 vyazozania usimamizi wa choo

Taifa Leo - - HABARI ZA KAUNTI - Na SAMMY KIMATU

VIKUNDI viwili vinang’ang’ania usimamizi wa choo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-kaiyaba, South B, Kaunti ya Nairobi.

Choo hicho kiko karibu na steji ya matatu katika barabara ya Enterprise kuelekea General Motors.

Wanachama wa kikundi cha Kaiyaba Young Single Mums kilivurunga shughuli katika mradi wa choo wa Biashara Pamoja Group Toilet (BPGT) na kulazimisha biashara kusimama kwa muda.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa BPGT, Dkt Kennedy Kipchumba, mradi wa choo hicho ulianza mwaka 2010 na kupitishwa na Baraza la Jiji kulingana na stakabadhi zilizotiwa saini na Bw P.T Odongo kwa niaba ya Katibu wa Jiji la Nairobi.

“Sisi ni wanachama 24 na hulipa Sh5,000 kila mwaka kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa miaka tisa sasa. Wakati huu serikali inapambana kumaliza ufisadi, twataka kujua ni nani anawapotosha na kuwalaghai wasichana hawa wa mtaani kwa kuwapa choo kilicho ni mradi wetu,” Dkt Kipchumba akafoka.

Kukundi cha Kaiyaba Young Single Mums kinadai kupewa barua kutoka afisi ya Gavana Mike Sonko wa Kaunti ya Nairobi na barua iliyotiwa saini na Bw Leboo Ole Morintat aliyedaiwa ni naibu wa katibu na Mkuu wa Huduma kwa Umma.

Katika barua hiyo (Taifa Leo inayo) kutoka afisi ya Gavana Sonko na kuandikiwa Kamanda wa Polisi wa Nairobi inaonyesha orodha ya vyoo 42 vya umma na waliopatiwa kandarasi ya kusimamia.

Hat hivyo, nakala ya mkuu wa kaunti ndogo ya Starehe imeandikwa kwa mkono, iko na stamou ya kuonyesha aliipokea lakini haijatiwa saini.

“Tunajua wanaongozwa na diwani mtarajiwa aliyebwagwa katika uchaguzi uliopita na anawatumia vijana vibaya,” mwanachama aliyetambuliwa kwa jina Bw Jubilee akasema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.