Amlima mume kugundua hakuwa na karo ya mwanao

Taifa Leo - - DONDOO! - NA CORNELIUS MUTISYA

Mama wa hapa alimtwanga mumewe alipogundua hakuwa amehifadhi pesa zozote za kulipa karo ya mwana wao.

Kulingana na mdaku wetu, polo alikuwa akichapa kazi Nairobi na akaritaya mwaka uliopita kutokana na kudhoofika kwa hali yake ya kiafya na akalipwa marupurupu yake yote.

Inasemekana polo alipofika nyumbani, alitumia pesa hizo kukarabati nyumba yake ya vyumba vinne ikawa ya kisasa na pesa zilizobaki, akazitumia kufurahisha ndugu na marafiki.

Twaarifiwa kuwa jamaa alisahau kabisa kuwa kitinda mimba wao alikuwa anajitayarisha kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.

'' Mtoto wa polo huyo alifanya vizuri sana katika mtihani wa KCPE. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliong'ara sana kitaifa,'' alisema mdokezi.

Inadaiwa kwamba, siku ambayo wanafunzi walitakiwa kujiunga na kidato cha kwanza ilipowadia, mama watoto alimuitisha polo pesa za karo na akasema hakuwa hata na senti moja mfukoni.

'' Mama watoto alikasirika sana mumewe alipomwambia peupe hakuwa na pesa za kugharamia masomo ya mwana wao na akaanza kumtupia cheche za matusi kabla ya kumchapa,'' asema mdaku wetu.

Duru zaarifu kuwa, polo alipoona hakuwa na lingine la kufanya, aliamua kuuza sehemu ya shamba lake na mtoto wao akaenda shuleni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.