Mbona serikali haijakomesha mauaji ya wazee Pwani?

Taifa Leo - - DIMBA - Na CHARLES WASONGA

UHAI ni kitu cha thamani mnamo kwa mwanadamu na kwa Mungu. Hii ndiyo maana moja kati ya amri kumi ambazo Mungu alimpa Musa ni kwamba, “Usiue”.

Na kulingana na sheria zote zinazotumika nchini, ikiwemo Katiba, hakuna mtu aliye na uhuru wa kuutoa uhai wa mwenzake.

Hii ndiyo maana katika mahakama zetu wale ambao hupatikana na hatia ya kutoa roho za wanadamu wengine, kimakusudi, hupewa hukumu kali, ikiwemo ya kunyongwa.

Lakini inasikitisha kuwa kuna watu fulani ambao wameamua kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuwaua wazee katika maeneo ya Kaunti za Kwale na Kilifi.

Miaka kadhaa iliyopita ilidaiwa kuwa wazee hao walikuwa wakiuawa kwa tuhuma za kuwa wachawi. Waliolengwa zaidi ni wazee wenye macho mekundu.

Na tangu mwaka jana, imeibuka kuwa wakongwe hao wanaangamizwa kwa kile kinachotajwa kama tamaduni za pwani ambazo, kwa hakika, hazieleweki.

Kuna wale wanaodai kuwa wazee hawa wanauawa kutokana na mizozo ya ardhi; eti wanaotekeleza mauaji hayo wanalenga kunyakua ardhi za wakongwe hao.

Nadharia hizi zote hazina msingi wowote na hazifai kutumiwa kama msingi wa kutekeleza unyama huu ambao unakwenda kinyume na kipengee cha 26 cha katiba, sheria ya uhalifu na amri ya Mungu.

Hii ndiyo maana ninaunga mkono tangazo la Waziri wa Masuala ya Ndani, Dkt Fred Matiang’i kwamba maafisa wa usalama watapambana vikali na wahusika wa uhalifu huu ambao umewatia hofu wazee katika eneo zima la Pwani mwa Kenya.

Ni wajibu wa serikali ya kitaifa kuhakikisha kuwa Wakenya, wa umri wowote, wanaishi katika mazingira salama bila kuhofia maisha yao.

Lakini inasikitisha kuwa siku chache baada ya Dkt Matiang’i kutoa onyo hilo, Mzee Zuma Ngome ambaye ni mkazi wa eneobunge la Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale alivamiwa na kuuawa kikatili na watu wasiojulikana.

Ilidaiwa kuwa waliomuua mzee huyo, mwenye umri wa 63, kwa kumkatakata kwa panga ni kundi fulani la vijana.

Kisa hicho kinapitisha ujumbe kwa Waziri Matiang’i, na walinda usalama kwamba wahalifu hawa hawajali mkono wa sheria na kwamba itakuwa vigumu kuwakamata.

Kwa hivyo, serikali inapaswa kubadili mbinu za kukabiliana na ukatili huu ambao huwaangamiza zaidi ya wazee 60 kila mwaka.

Kwa mfano, serikali ishirikiane na mashirika ya kutetea maslahi ya wazee kama vile Helpage, kutoa hamisisho na mafunzo kwa wanajamii kwamba kuna njia mbadala za kusuluhisha mizozo ya ardhi wala sio kuwaua wazee.

Vijana wanaowaua wazee wanapaswa kufahamishwa kwamba wanaweza kuwasilisha lalama zao kwa afisi za Wizara ya Ardhi na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) badala ya kuwaua wazee.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.